WALIMU wa Shule ya Msingi Buguruni Viziwi, iliyoko Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, wameishukuru serikali kwa kuwapatia wanafunzi wao elimu ya usalama barabarani, inayowalinda na ajali za barabarani.
Wamesema kabla ya kutolewa elimu hiyo, walikuwa wakiacha shughuli zao za ofisini na kwenda kuwavusha wanafunzi.
Mkuu wa shule hiyo, Yahya Maftah, aliyasema hayo jana, alipozungumza na gazeti hili na kuongeza kuwa, ajali nyingi zimekuwa zikitokea shuleni hapo kutokana na wanafunzi kutokusikia vizuri.
“Hali hiyo inatokana na wanafunzi wanapovuka barabara pamoja na madereva kuwapigia honi, ilikuwa kazi bure na pengine kuwaona wana jeuri, bila kujua wana tatizo la kutosikia vizuri,” alisema.
Alisema mbali na kuwepo kwa alama za barabarani katika eneo hilo, kulikuwa na utaratibu wa kuwepo polisi wa usalama barabarani, kwa lengo la kuwapatia wanafunzi hao elimu ya kujikinga na ajali za barabarani.
Aliongeza kuwa walianzisha utaratibu wakiamini ungewasaidia wanafunzi hao pindi wanapovuka barabara, kwa kuwapatia vibao na vifaa maalumu vya kuakisi mwanga, kwa ajili ya kuwaongoza kuvuka barabara.
“Wanafunzi walikuwa wakiandika namba zote za magari, ambazo wakati wakifanya shughuli yao ya kuvushana barabarani, yalipita na kuharibu utaratibu na kuripoti tatizo hilo kwangu, yasihatarishe maisha yao,” alisisitiza.
Alibainisha kwamba kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na serikali, ikiwemo kuwapatia wanafunzi elimu, zimesaidia kupunguza ajali za barabarani.
Mkazi wa Buguruni Malapa, Boniface Richard, alisema hatua ya wanafunzi hao kutumia riflekta na vibao wakati wa kuvuka barabara, imesaidia madereva wengi kuwa waangalifu wakati wanapovuka.
Na Habiba Msemo (DSJ)





























