BUNGE limeelezwa mikakati iliyofanya ya udhibiti mapato yatokanayo na gawio imewezesha kuongeza makusanyo ya gawio kutoka sh. bilioni 34.92 mwaka 2015/2016 hadi kufikia sh. bilioni 155.10 mwaka 2020/2021.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, ametoa kauli hiyo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Jesca Kishoa.
Katika swali lake, mbunge huyo alihoji serikali inatumia mikakati gani kudhibiti mapato yatokanayo na gawio kutoka katika kampuni ambayo serikali inamiliki hisa chini ya asilimia 50.
Akijibu swali hilo, Dk. Mwigulu amesema kiasi hicho cha gawio ni kutoka kampuni ambazo zina hisa chache.
Alifafanua kuwa serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina ambaye ndiye msimamizi wa uwekezaji wa serikali katika taasisi na mashirika ya umma pamoja na kampuni ambazo serikali ina hisa chache, inadhibiti mapato yatokanayo na gawio.
Alieleza mikakati hiyo ni kuhakikisha kuwa kila kampuni ina sera ya gawio, kurejea kwa mikataba ya mauzo ya hisa katika kuhakikisha maslahi ya serikali yanalindwa pamoja na kufanya uchambuzi wa mara kwa mara kuhusu utendaji wa taasisi hizo.
Aidha, alisema serikali ina uwakilishi katika bodi za wakurugenzi wa kampuni ambapo pamoja na mambo mengine zinasimamia maslahi ya serikali katika kampuni ikiwa ni pamoja na malipo ya gawio.
Na SELINA MATHEW, Dodoma



























