JESHI la Polisi Mkoa wa Ilala linamshikilia askari Magereza, Said Hassan, (26) Mkazi wa Ukonga Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kubaka na kulawiti binti wa miaka 29.
Limesema mtuhumiwa huyo mwenye namba za usajili B9780 WDR alitenda kosa hilo Septemba Mosi, mwaka huu saa 5:30 usiku Ukonga Madafu akiwa na mwenzake ambaye bado hajakamtwa.
Akizungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Debora Magiligimba, amesema mtuhumiwa huyo kwa kushirikiana na mwenzake mmoja, walimkamata kinguvu binti huyo na kwenda nae katika nyumba iliyokuwa jirani na kambi ya Ukonga Magereza huku wakimbaka na kumlawiti kwa zamu.
“Mnamo tarehe Moja Septemba majira ya saa tano na nusu usiku, katika barabara ya Madafu Ukonga mtuhumiwa huyo ambaye ni askari wa Jeshi la Magereza mwenye namba B9780 WDR Said Hassan walimkamata kinguvu msichana huyo na kisha kuondoka naye hadi katika nyumba iliyokuwa jirani na kambi,”amesema.
Pia Kamanda Magiligimba alisema kuwa watuhumiwa hao baada ya kumlawiti na kumbaka binti huyo, waliendelea kumfanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia na kumsababishia majeraha na maumivu sehemu za siri.
Aidha, Kamanda Magiligimba alisema mtuhumiwa baada ya kugundua anatafutwa na Jeshi la Polisi alijaribu kujinyonga na kuacha ujumbe wa maandishi kwa mkuu wake wa kazi na askari wenzake, lakini kabla ya kufanikisha azma yake alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi.
Kamanda Magiligimba, alisema mtuhumiwa huyo aliacha ujumbe uliosomeka “Mnisamehe bure kwa uamuzi wangu niliochukua kwa tukio nililolifanya nitaonekana nimekufa kizembe”.
Aidha Kamanda Mgiligimba alisema Jeshi la Polisi Ilala linaendelea na msako mkali kumkamata mtuhumiwa mwingine aliyekimbia baada ya kufanya tukio hilo.
Na IRENE MWASOMOLA



















