MABONDIA 18 wanatarajiwa kupanda ulingoni kwa uzito tofauti utakaofanyika Septemba 26 mwaka huu katika Uwanja wa Tegeta Nyuki , Dar es Salaam.
Pambano hilo maalumu lina lengo la kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, juu uchomaji wa chanjo ya Uviko-19 .
Akizungumza na UhuruOnline, Mratibu wa pambano hilo, Salumu Viduka, amesema mchezo wa ndondi una mashabiki wengi hivyo kupitia idadi hiyo itakuwa njia nzuri ya kuhamasisha wananchi kuchoma chanjo ya UVIKO-19 ili kuepukana na maambukizi .
“Mapambano yatakuwa tisa kati ya hayo moja litahusisha wanawake, lakini mpaka sasa bondia, Agnes Kayage, hajapata mpinzani bado tunamtafuta,” amesema Viduka
Mratibu huyo ameeleza kuwa, mabondia wote wanaendelea na mazoezi ili kujiandaa vilivyo na pambano hilo na kuonyesha burudani nzuri kwa mashabiki.
“Tunawaomba mashabiki na wapenzi wa ndondi kujitokeza kwa wingi katika pambano hili, ili kushuhudia burudani kali na kuchoma chajo, “ ameongeza Viduka.
Viduka ametaja baadhi ya mabondia watakaopanda ulingoni ni Alex Kachelewa atazichapa na Hashim Chisola, Philipo Okololo atapigana na Gerad Mohamed , Jackson Mkude dhidi ya Beda Thomas na Ramadhan Chicha anacheza Ahmed Kelebela .
Na AMINA KASHEBA