IKIWA imebaki siku moja wanafunzi wa Darasa la Saba kufanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu Elimu ya Msingi Waziri wa Elimu Sayasi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, amewataka wasimamizi wa mitihani kujiepusha na vitendo vya udanganyifu ikiwemo kuvujisha mitihani.
Onyo hilo amelitoa leo wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea shule ya Sekondari ya mfano ya Iyumbu iliyopo eneo la Iyumbu jijini Dodoma ili kuona maendeleo ya ujenzi huo.
Amesema katika miaka miwili iliyopita kumekuwa na tabia na vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na wasimamizi wa mitihai ya taifa katika shule mbalimbali ndiyo maana kumekuwa na usimamizi mkali ikiwemo askari.
“Nimeona nikumbushe na kutoa onyo kwa wasimamizi wenye tabia hii, kuacha mara moja ili kuweka heshimu kwa taaluma ya walimu nchini, wafanye kazi hiyo kwa weledi na uaminifu mkubwa maana wameaminiwa,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali imejipanga na itahakikisha watu wote
watakaohusika na kushiriki katika vitendo hivyo vya udanganyifu
wanabainika na kuchukuliwa hatua kali za kisheria na kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine.
“Wasimamizi wote wanapaswa kufuata utaratibu na kanuni za usimamizi, katika mitihani ya Taifa naomba wasimamizi wote mfanye kazi ya usimamizi kwa weledi ili wanafunzi watahiniwa wafanye mitihani sahihi kwa kutumia akili zao na uwezo waliofundishwa darasani,” amesema.
Aidha, amewataka watahiniwa kujiamini wanapoingia katika chumba cha mtihani hiyo ya Taifa ili waweze kufanya vizuri na kupata ufaulu mkubwa, kwa sababu serikali hivi sasa imewekeza katika suala la elimu kwa kiasi kikubwa.
Na Happiness Mtweve, Dodoma





























