MKUU wa Kikosi maalum cha Jeshi kilichompindua Rais Alpha Conde, Kanali Mamady Doumbouya amesema maofisa wa serikali ya Guinea sasa hawatoruhusiwa kusafiri nje ya nchi huku akimtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Ibrahima Kassory Fofana na maofisa wengine kurejesha magari waliyokuwa wanayatumia.
Kanali Doumbouya pia ametangaza kuondoa marufuku ya kutotoka nje katika maeneo yaliyo na migodi na wananchi wanapaswa kuendelea na shughuli zao katika maeneo hayo, huku akiwataka wananchi waendelee kuwa na utulivu.
Kanali Doumbouya amekiambia kikao cha mawaziri wa Conde akiwemo Waziri Mkuu na maofisa wengine wakuu serikalini amesema “Umasikini na ufisadi uliozagaa ndivyo vilivyopelekea vikosi vyake vimng’oe madarakani Rais Alpha Conde”.
Mapinduzi hayo katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi iliyo na utajiri mkubwa wa madini ya bauxite ambayo yanatumika kutengeneza chuma cha pua yamesababisha bei ya chuma hicho kuongezeka na kufikia bei ambayo haijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 10.
Hata hivyo, hadi jana vikosi vingine vya kijeshi nchini Guinea bado havijatoa tamko kuhusu mapinduzi hayo yaliyofanyika huku Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ikiendelea kusisitiza kuwa hakuna mapinduzi yaliyofanyika nchini hapo.
Vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo televisheni ya CNN ya Marekani na shirika la habari la Xinhua la China vimenukuu taarifa ya serikali ya Guinea ikidai kwamba jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuzima uasi wa wanajeshi waliotangaza kupinduza serikali.
Kwa mujibu wa Xinhua, Wizara ya Ulinzi ya Guinea imesema katika taarifa yake rasmi, kikosi maalumu cha ulinzi wa Rais kimefanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi na kuwarudisha nyuma wanajeshi waasi.
Sambamba na taarifa ya wizara ya ulinzi ya Guinea kuthibitisha kutokea mapigano makali mjini Conakry, imesema kuwa, wanajeshi waasi wamesababisha hofu na matatizo ya kiusalama kwa watu wanaishi karibu na Ikulu.
Kwa upande wake na katika habari ya karibuni, televisheni ya Al Jazeera imetangaza wanajeshi waasi wametangaza amri ya kutotoka nje katika maeneo yote ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
CONAKRY, Guinea