SIKU chache baada ya bondia namba moja Tanzania na Afrika wa ngumi za kulipwa, Hassan Mwakinyo, kupanda kiwango katika rekodi ya boxrec, Emmanuel Mlundwa, amesema hatua hiyo itakuza mchezo wa ndondi nchini.
Mwakinyo ambaye ana nyota nne juzi alipanda kiwango kutoka nafasi ya 24 hadi 13 baada ya kumchakaza mnamibia, Julius Indongo, kwa TKO raundi nne katika mchezo wa raundi 12 uzani wa kilo 69 pambano lililofanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Akizungumza na mwandishi wa UhuruOnline, Mlundwa ambaye ni bondia nguli mstaafu, amesema tunampongeza Mwakinyo kwa hatua aliyofikia kwasababu amefikia mahali ambapo anacheza na bondia yoyote duniani.
‘Pongezi kwa Mwakinyo kwa hatua aliyofikia kwani sasa anaweza kupigana na bondia yoyote duniani, pia wakati huu anatakiwa kuongeza juhudi ili kufikia nafasi ya tano kwa ajili kucheza hata bingwa wa dunia, ‘ amesema Mlundwa.
Mkongwe huyo ameeleza katika kupanda kiwango hicho kuna faida na hasara kwa bondia huyo.
‘Tunafurahi kuona Mwakinyo anawakilisha taifa na kupeperusha vema bendera ya nchi, lakini uoga wangu kwa Mwakinyo kunyimwa hiyo nafasi na mabondia mwenye sifa zaidi yake watakataa kuja kucheza hapa nchini mwishoni atashuka kiwango kama ilivyokuwa kwa bondia Mbwana Matumla, ‘ amesema Mlundwa.
Mlundwa amefafanua kuwa, bondia Matumla alifanikiwa kupanda kiwango cha nafasi ya tatu kipindi cha miaka 10 iliyopita ila alishuka kiwango kutokana na kukosa kucheza mapambano ya ubingwa wa mikanda mikubwa kama WBC, IBF na WBA.
Kocha wa Mwakinyo, Amos Nkondo ‘Amoma’ amesema sasa wana mikakati na mipango ya kumuandaliwa mapambano ya nje ya nchi ili kuongeza ufanisi katika mchezo wa ndondi.
Amoma ameeleza lengo la kumuandaliwa mapambano ya kimataifa ni kutokana na nafasi aliyokuwa nayo ili kuongeza ubora zaidi.
‘Mkakati na mipango ni kumuandalia mapambano ya kimataifa katika ngumi zilizopozaliwa kama Canada, USA na Afrika Kusini na nchi ambazo zinazoendelea na ndondi ili aende kushindana, ‘ amesema Amoma.
Na AMINA KASHEBA