BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA), limetangaza kuanza rasmi kwa mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi kwa mwaka huu kote nchini, huku likitahadharisha wadau dhidi ya vitendo vya kuvujisha mitihani.
Limesema mitihani hiyo inayoanza kesho na kutamatishwa keshokutwa, inafanyika katika vituo 17,585 vikiwemo vinane, ambavyo vilisimamishwa miaka minne iliyopita kama adhabu baada ya kubainika kuwa vilijihusisha na wizi wa mitihani.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake Mikocheni mkoani Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, amesema vitendo vya uvujishaji wa mitihani ya taifa havina tofauti na uhujumu wa uchumi wa nchi.
Kauli ya Katibu mtendaji huyo wa NECTA, imekuja siku moja baada Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, atoe wito kwa wasimamizi wa mitihani inayoanza hapo kesho kujiepusha na udanganyifu ikiwemo kuivujisha.
Dk. Msonde amesema kwa mwaka, shughuli za mitihani zinagharimu serikali mabilioni ya fedha, hivyo kundi lolote linapojaribu kuvujisha mtihani wowote, ni sawa na kuhujumu kwa makusudi uchumi.
Amesema katika uchunguzi uliofanywa na NECTA kwa miaka kadhaa, imebainika kuwa makundi makuu ambayo yanahusika moja kwa moja na uvujishaji wa mitihani ni wamiliki wa shule, waratibu elimu kata na walimu wakuu wa shule husika.
“Baraza la mitihani linawaasa walimu wakuu, waratibu elimu kata na wamiliki wa shule, kutojihusisha katika kupanga na kutekeleza njama za udanganyifu… NECTA hatutasita kumchukulia hatua yeyote atakayebainika kuhusika kusababisha udanganyika kwenye shule yeyote,” amesema.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka wamiliki wa shule zinazotumiwa kufanyia mitihani kutambua shule hizo kwa siku mbili kuanzia leo, ni vituo maalumu vya mitihani na kwamba hawatakiwa kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani hiyo.
Msonde amesema NECTA hawatasita kukifutia usajili kituo chochote cha mitihani, endapo watajiridhisha bila shaka, kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa mitihani ya taifa ambayo inaendelea katika shule husika.
MAANDALIZI YA MTIHANI
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mtihani huo, Katibu mtendaji huyo amesema , maandalizi yamekamilika na kwamba mitihani imeanza kutawanywa kwa ajili ya kuanza kwa ratiba leo.
Dk. Msonde amesema kwa mwaka huu, jumla ya wanafunzi 1,132,143 wanatarajiwa kufanya mtihani huo na kwamba kati ya hao, wasichana ni 584,641 sawa na asilimia 51.64 na wavulana ni 547,502 ambao ni asilimia 48.36 ya watahiniwa wote.
Kadhalika amesema katika watahiniwa hao waliojisajili kwa mwaka huu, watahiniwa 1,079,943 watafanya mtihani kwa lugha ya kiswahili huku watahiniwa 52,200 wakitarajiwa kufanya mtihani huo kwa lugha ya kiingereza.
“Aidha watahiniwa wenye mahitaji maalumu wapo 3,327 kati yao wasioona ni 108, wenye uoni hafifu 951, wenye uziwi 739, wenye ulemavu wa akili 358 na 1,171 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili,” amesema Dk. Msonde.
KUONGEZEKA KWA MASOMO
Vilevile, Msonde amesema katika mtihani wa mwaka huu, masomo yanayofanyiwa mtihani yameongezeka kutoka matano hadi sita, kufuatia kuongezeka kwa somo la Uraia na maadili, mabadiliko yaliyotokana na utekelezaji wa mtaala uliotumiwa na wanafunzi hao, tangu walipoanza darasa la kwanza.
Mbali na ongezeko hilo, amesema mabadiliko mengine yaliyosababishwa na utekelezaji wa mtaala, ni maboresho ya maudhui ya masomo mawili ambayo ni Sayansi hivyo kubadilishwa jina na kuwa Sayansi na Teknolojia na somo la Maarifa ya Jamii, ambalo katika mtihani huu linaitwa Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi.
Kufuatia maelekezo hayo ya NECTA, UhuruOnline imetembelea shule kadhaa za msingi jijini Dar es Salaam, ikiwemo shule ya Mnazi Mmoja, Lumumba, Mwalimu Nyerere (zamani Makurumla) na Shule ya Msingi Turiani, na kukuta maaandalizi yakiwa yamekamilika.
Maandalizi hayo ni pamoja na kuandaliwa kwa vyumba vya kufanyia mitihani, kupangwa kwa samani zilizobandikwa namba ya kila mtahiniwa na usalama wa jumla wa eneo, ambapo baadhi ya shule zimefungwa kamba maalumu na kubandikwa mabango yanayoeleza kuwa si ruhusa kwa mtu kupita karibu na eneo hilo.
Na WILLIAM SHECHAMBO



























