MKAZI wa Tegeta, Dar es Salaam, Kelvi Kelvin, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni, akikabiliwa na shtaka la mauaji.
Kelvin (29) alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka na Wakili wa Serikali, Benson Mwaitenga, mbele ya Hakimu Mkazi, Sifa Jacob.
Wakili Mwaitenda alidai mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo, Julai 21, mwaka huu, eneo la Tegeta Magereji, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo kwa makusudi alimuua Isaa Said.
Hakimu alimweleza mshitakiwa huyo kuwa hatakiwi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Mshitakiwa alirudishwa rumande hadi Septemba 17, mwaka huu, shauri litakapopelekwa kwa kutajwa.
Wakati huo huo, mkazi wa Manzese, Ubungo, Dar es Salaam, Husna Rashid (27), alifikishwa mahakamani hapo kujibu shtaka la kusafirisha kilogramu 37.2 za dawa za kulevya aina ya bangi.
Wakili wa Serikali, Vaileth David, alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Lilian Silayo, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo, Agosti 28, mwaka huu, eneo la Manzese Uzuri.
Alidai mshitakiwa siku hiyo alikutwa akisafirisha dawa hizo za kulevya. Hata hivyo, Husna alikana kutenda kosa hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu alimweleza mshtakiwa huyo kuwa shauri linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria kutokana na kiwango kikubwa cha dawa za kulevya anachodaiwa kukutwa nacho, hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 22, mwaka huu.
EVODIA MICHAEL (UDSM) NA HAWA NGADALA



























