MKAZI wa Bunju, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Mongela Mtago, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kwa shtaka la ubakaji.
Mtago (29) alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka na Wakili wa Serikali, Michael Shindai, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Aaron Lyamuya.
Wakili Shindai alidai, mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Januari Mosi na Mei 29, mwaka huu, eneo la Bunju, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam ambapo kwa makusudi alimbaka binti mwenye umri wa miaka 16.
Mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamuhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu alitoa masharti ya dhamana kwa mshitakiwa yaliyomtaka awe na wadhamini wawili watakaotia saini bondi ya sh.milioni mbili kila mmoja.
Mshitakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti hayo na shauri liliahirishwa hadi Septemba 20, mwaka huu, kwa usikilizwaji wa awali.
EVODIA MICHAEL (UDSM) NA HAWA NGADALA



























