UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, umesema mikutano ya kusikiliza kero iliyofanywa wilayani humo na Mkuu wa Mkoa Amos Makalla, imeongeza kasi ya kutafutiwa ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.
Pia, umoja huo umesema hatua hiyo, imekisaidia Chama Cha Mapinduzi, kupunguza mzigo wa kujibu maswali ya changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi.
Katibu wa UVCCM, Wilaya ya Temeke, Andrew Gwaje, aliyasema hayo, alipozungumza na UhuruOnline na kusema kuwa mikutano hiyo imekuwa na tija kwa serikali, wananchi na Chama kwa ujumla.
Gwaje alisema utaratibu huo umetoa fursa kwa wananchi kutoa kero zao ana kwa ana, tofauti na utaratibu wa kumfuata mkuu wa mkoa ofisini kwake.
“Mikutano ya mkuu wa mkoa kusikiliza kero iliyofanyika wilayani kwetu imewarahisishia wananchi kutoa kero zao na Chama imetupunguzia maswali ambayo tungeulizwa na wananchi katika kuwatatulia,” alisema.
“Pia imewarahisishia wananchi kama wangetaka kumpata mkuu wao wa mkoa ofisini kwake, wangemsubiri muda mrefu au kuambiwa hayupo, lakini katika mkutano wanamuona kwa urahisi na kutoa kero zao,”alisema.
Aidha, alisema mikutano hiyo imewasaidia wananchi kuwafahamu wanasheria wa manispaa hiyo na maofisa wa kada mbalimbali wanaohusika moja kwa moja na kero zao.
Gwaje alimpongeza mkuu wa mkoa huyo kwa utaratibu wa kujibu maswali ya wananchi kwa kuwaita maofisa wa manispaa kujibu changamoto zinazoelekezwa katika idara wanazoongoza.
Alitoa mfano wa mkutano uliofanyika uwanja wa Mwembeyanga, ambapo kila kero ilijibiwa na maofisa wa manispaa hiyo kwa hatua za ufuatiliaji na utekelezaji.
Gwaje alisema changamoto nyingi zilizotolewa na baadhi ya wananchi katika mikutano hiyo, zilielekezwa katika ajira na migogoro ya ardhi.
Katibu huyo alishauri viongozi wa manispaa kushughulikia changamoto za wananchi na aliwapongeza wakazi wa wilaya hiyo waliojitokeza katika mikutano hiyo na kuomba iwe endelevu.
Na SIMON NYALOBI



























