NAIBU Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, amesisitiza msimamo wa serikali kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme ni sh. 27,000 na hakuna gharama ya nguzo, nyaya wala mita.
Pia Byabato amesema watachukua hatua dhidi ya maofisa wa TANESCO ambao watabainika kuwaunganishia wananchi umeme kwa bei zaidi ya sh. 27,000.
Kauli hiyo ya serikali inakuja baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuhusu kupandishiwa gharama za kuunganishiwa huduma hiyo, kwa kigezo cha kuwa mbali na nguzo.
Akizungumza na UhuruOnline, Byabato amesema maelekezo ya serikali ni kwamba, nguzo, nyaya na mita hazilipiwi na mwananchi anapohitaji kuunganishiwa huduma.
Amebainisha kuwa, wakati serikali inapanga gharama hiyo ilifahamu uwepo wa baadhi ya wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyoko mbali na nguzo za umeme, hivyo kisiwe kigezo cha kuongezewa gharama za kuunganishiwa huduma.
“Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limejizatiti kuhakikisha linaboresha huduma zake na kuwaunganishia wananchi huduma kwa gharama pendekelezwa, hakuna gharama zaidi ya iliyopo,” amesema.
Ameongeza kuwa, maelekezo ya serikali kupunguza gharama ya kuwaunganishia wananchi umeme, yalilenga kuwapunguzia mzigo ili kila mmoja anufaike.
Byabato ameagiza aliyelipishwa gharama ya nguzo au kuongezewa gharama ya kuunganishiwa huduma kwa madai ya kuwa mbali na nguzo atoe taarifa ili hatua zichukuliwe.
“Siku zote nimekuwa nikiomba kielelezo cha mmoja aliyeomba kupewa hela zaidi ya sh. 27,000 kwa ajili ya kuunganisha umeme, popote itakapotokea naomba taarifa za huyo mtu awe mfano kwa wengine,” alisema.
Alisisitiza hatua zitachukuliwa kwa ofisa anayetoza wananchi gharama ya nguzo wakati wa kuunganisha umeme.
Awali akiungumza na UhuruOnline, Anthony Munyigo, mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam, alisema baba yake alikwama kuunganishiwa umeme kutokana na kuwa mbali na nguzo.
Alisema kwa sababu hiyo, alimtaka kugharamia sh. 300,000 badala ya 27,000 ili kuunganishiwa huduma hiyo, ambapo gharama hiyo inahusisha na nguzo.
Aliongeza baada ya kulalamika na kwenda katika ngazi mbalimbali za serikali ndipo baba yake aliunganishiwa huduma hiyo kwa sh. 27,000.
Na JUMA ISSIHAKA



























