MGOMBEA wa ubunge, Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amevitaja vipaumbele vitano atakavyoanza kuvitekeleza, atakapopata ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi katika jimbo hilo.
Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni sekta za elimu, afya, maji, umeme na miundombinu ya barabara ili kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo wanaondokana na changamoto hizo.
Hayo ameyasema katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Igunda, alipokuwa akiomba kura kwa wananchi.
Ameahidi endapo atapata ridhaa hiyo atahakikisha wananchi wa Jimbo hilo wanaondokana na changamoto hizo kwa kushirikiana na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Cherehani alisema changamoto hizo zimekuwa zikiwakwamisha wananchi kufikia malengo yao katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
“Naombeni kura zenu niwalipe maendeleo. Mimi ni mzaliwa wa Ushetu, matatizo yenu nayajua, nitahakikisha kila aliyepewa dhamana ya kutatua changamoto za wananchi anatimiza wajibu wake kama inavyotakiwa,” alisema Cherehani.
Alifafanua kuwa kipaumbele chake namba moja ni sekta ya elimu, ambapo kwa kushirikiana na serikali atahakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia, upatikanaji wa vifaa na uwepo wa walimu wa kutosha katika shule za msingi na za sekondari.
“Kipaumbele cha pili ni afya nitahakikisha natatua changamoto zinazowakabili wananchi hususan upatikanaji wa dawa na vifaa tiba,” alisema na kutaja kipaumbele cha tatu kuwa ni maji ambapo atahakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa kuchimba visima huku wakiendelea kusubiri mradi mkubwa wa maji ya ziwa Victoria.
Aliongeza kuwa kipaumbele chake cha nne ni umeme, ambapo atahakikisha maeneo yote ambayo hayajapata huduma ya nishati yanafikiwa ili kuongeza uzalishaji mali kupitia uanzishwaji wa viwanda.
“Kipaumbele changu cha tano ni miundombinu ya barabara endapo nikichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hili nitahakikisha naishawishi serikali kujenga barabara mpya katika maeneo ambayo hayapitiki,” alisema
Alieleza kuwa atafanya hivyo ili kutoa fursa kwa wananchi kusafirisha mazao yao na kuwaomba kumpigia kura.
Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kahama, Thomas Myonga, aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua mgombea ubunge Cherehani anayetokana na CCM kwa kuwa ni Chama kina ilani inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita.
Na SALVATORY NTANDU, USHETU