WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo, amemuagiza uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani, kuandaa mpango mkuu wa kuboresha majengo na kuyaondoa ya zamani yaliyojengwa tangu mwaka 1954.
Amesema majengo hayo yamechoka na kwamba lengo la mpango huo ni kutengeneza mazingira ya huduma zote za afya za msingi ili zipatikane hapo.
Jafo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kisarawe ametoa agizo hilo, Wilayani Kisarawe, alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo likiwemo la huduma za mama na mtoto, ambapo sh. milioni 900 zilitolewa kwa kazi hiyo.
Hayo aliyafanya wakati akiongoza Maadhimisho ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa Pwani yaliyofanyika kimkoa Wilayani Kisarawe.
Amesema mpango mkuu huo uende na mkakati wa kujenga majengo mapya ya ghorofa yatakayojengwa katika mpangilio mzuri na kuyaondoa majengo yote ya zamani na kujengwa kwa mfumo wa ‘force account’ ambao ni ujenzi wa gharama nafuu.
“Sifikirii kutafuta fedha za ukarabati wa majengo ya zamani ambayo mafanikio yake ni madogo isipokuwa mkakati uwe wa kutafuta fedha za majengo mapya ya ghorofa na kuondoa majengo yote ya zamani,” amesema Jafo.
Alieleza lengo la kukamilika kwa ujenzi wa hospitali mpya lengo ni kukabiliana na idadi kubwa ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Temeke na Hospitali Teule ya Tumbi.
“Tutahangaika kutafuta fedha maana serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, haishindwi kupata fedha za ujenzi huo wa hospitali ili hayo majengo mengine tuyaondoe tunataka wagonjwa wanaokwenda Dar es Salaam na Kibaha, hata wagonjwa wa Chanika, Majohe waje hapa kupata huduma,” alisema Jafo.
Aliongeza kuwa: “Tukiijenga hospitali hii vizuri najua itasaidia kupunguza kazi ngumu ya kampeni za uchaguzi mkuu ujao mwaka 2025 kwa sababu wananchi wa kawaida watapata huduma zote bora hapa hapa Kisarawe.”
Awali, Mwenyekiti wa UWT, Mkoa wa Pwani, Farida Mgomi, alisema Umoja huo umekuwa katika maadhimisho hayo ya wiki ya kuzaliwa kwa UWT nchini kwa kufanya matukio mbalimbali ya kijamii katika wilaya zote za Mkoa wa Pwani.
Kilele hicho cha maadhimisho ya kuzaliwa UWT mkoani humo kilitanguliwa na matukio ya kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe na Shule ya Sekondari Kimani na kutoa misaada mbalimbali kwa wanafunzi.
Na Scolastica Msewa, Kisarawe



























