BAADA ya mapumziko ya siku mbili kikosi cha timu ya Simba kimeanza mazoezi, kwa ajili ya kujianda na mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Simba itakuwa mgeni katika mchezo huo utakaochezwa Oktoba 17, mwaka huu, kabla ya kurudiana Oktoba 22 katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Mkapa, Jijini Dar es Salaam.
Wabotswana hao walianzia hatua ya awali ambapo walifanikiwa kuiondosha Zilimadjou kutokea Visiwa vya Comoro kwa jumla ya ushindi wa mabao 5-1 katika mechi mbili walizocheza.
Akizungumza na UhuruOnline, Kocha wa Simba, Didier Gomes, alisema wameanza maandalizi ya mchezo huo mapema ili kuhakikisha kikosi kinakuwa imara tayari kwa ajili ya mchezo huo.
Alisema anatambua kwamba mechi za ugenini huwa ni ngumu na zenye changamoto mbalimbali, lakini wameanza kujipanga mapema ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Aliongeza kwamba wameanza mazoezi mapema ili kujenga kikosi cha ushindani kwa ajili ya kuwakabili wapinzani wao na kuhakikisha wanarejea nyumbani na ushindi.
“Ninatambua mechi za ugenini zina changamoto zake, hivyo tumeanza maandalizi ya mapema ili kuhakikisha tunashinda na kurejea nyumbani na pointi tatu ambazo ni muhimu kwetu.
“Tumeanza mazoezi na wachezaji waliobaki kwani wengine waliitwa katika timu za Taifa kwa ajili ya mechi zilizopo katika Kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hao tutaungana nao baadaye,” alisema Gomes.
Gomes alisema, atahakikisha anawanoa zaidi wachezaji waliobaki na kuwajenga kisaikolojia, ili wawe fiti kupambana na wapinzani wao.
Hata hivyo Gomes alisisitiza, atarekebisha makosa aliyoyaona katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara, ili kuhakikisha anayamaliza na timu ipate ushindi mnono ugenini.Wachezaji 16 wa kikosi hicho ndio wameitwa katika timu zao za taifa ambapo tisa wamejumuishwa Taifa Stars wakati saba ni wale wa kimataifa ambao wameitwa na mataifa yao.
Wachezaji hao ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Israel Mwenda, Erasto Nyoni, Kennedy Juma, Mohamed Hussein, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, John Bocco na Kibu Denis.
Wengine ni Meddie Kagere, Peter Banda, Duncan Nyoni, Joash Onyango, Rally Bwalya na Henock Banka.
Simba ilinza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kutoka suluhu dhidi ya Biashara United kabla ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa pili dhidi ya Dodoma Jiji.
Na NASRA KITANA