MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango, ameihakikishia Jumuiya ya Wanawake ya chama hicho (UWT) kuwa wao ni jeshi kubwa, hivyo wasibabaishwe na vyama vidogo vidogo vya upinzani.
Pia, amewashauri wasijiingize katika makundi yasiyofaa ambayo yanaweza kudhoofisha chama na jumuiya yao, wanapaswa kudumisha upendo, umoja na mshikamano.
Akizungumza Dar es Salaam katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya UWT iliyofanyika Viwanja vya Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Dk. Mpango alisema wanawake wana kila sababu kuhakikisha jumuiya yao, inaimarika na kuongeza wanachama wapya.
Aidha, aliwataka ndani ya jumuiya hiyo, kuwa makini na waepuke migogoro ambayo haina tija ndani ya chama.
Hata hivyo, Dk. Mpango aliwataka wanawake kujipanga kwa ajili na kujiandaa na chaguzi zitakazofanyika mwakani ndani ya chama na jumuiya zake, hivyo wanapaswa wawe makini kwa kuwatafuta wagombea waadilifu na wenye kuipenda CCM na wanachama wake.
Katika wiki hiyo ya kilele, Dk. Mpango aliwakumbusha UWT kuwa wabunifu ili kutafuta vyanzo vipya vya upatikanaji mapato.
Pia, Makamu wa Rais aliwakumbusha UWT, kujiandaa kuhesabiwa ili kupatikana takwimu sahihi ya wakazi, wanachama na jumuiya zake.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba, alimuondoa hofu Dk. Mpango kwa kumwambia Jumuiya hiyo ipo makini, ina weledi na inatekeleza maagizo yanayotoka ngazi ya juu ya chama kwa kiwango kinachoridhisha.
“Tunaipongeza Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Taifa kwa kupendekeza jina lako na kuwa mlezi, hawakufanya makosa, tunakuhakikishia tutakupa ushirikiano kwa yale yote unayohitaji katika kuimarisha chama,” alisema Kate.
Vilevile, Katibu wa Jumuiya hiyo, Grace Haule alisema ifikapo mwaka 2025, katika kampeni za Uchaguzi Mkuu, hawatafanya makosa, watakwenda na kaulimbiu yao inayosema; ‘Watasimama na Rais Samia Suluhu Hassan.’
“Salamu hizi kwa ajili ya wanawake wote wa mkoa huu, kwamba ushindi utapatikana kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Na REHEMA MAIGALA



























