WANANCHI wa Mkoa wa Dar es Salaam, wameshauriwa kuchukua tahadhari kuepuka athari za joto kali linalotarajiwa kuendelea kuongezeka kipindi hiki kinachokaribia kuanza kwa msimu wa mvua.
Pia, watu wenye umelemavu wa ngozi na wazazi wenye watoto wadogo, wameshauriwa kukaa kwenye maeneo yanye hewa ya kutosha na kutumia vikinga joto na jua vya kuwakinga na mionzi na kunywa maji ya kutosha ilikuepuka athari.
Akizungumza na UhuruOnline, mchambuzi wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Joyce Makwata, amesema joto linatarajiwa kuongezeka zaidi kuelekea msimu wa mvua za vuli, ambazo zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi huu.
“Katika kipindi kama hiki, joto kuanza kupanda ni kawaida na kusababisha kuwepo hali ya fukuto, ikiwa ni sehemu ya kuanza kunyesha kwa mvua,” ameeleza.
Amesema baada ya kumalizika kwa kipindi cha baridi, ambacho huwa kati ya mwezi Juni hadi Agosti, hali ya fukuto ya joto uanza hadi mwisho wa mwezi wa Oktoba ambapo mvua huanza kunyesha.
“Inapofikia kipindi cha mwezi Novemba, huwa hali ya joto inaongezeka zaidi tena kutokana na kuwepo jua la utosi,” amesema.
Mchambuzi Joyce amesema mvua hizo zinatarajiwa kunyesha katika mikoa mbali mbali ya nchi, ikiwemo, Dar es Salaam, Pwani, Kagera na mingineyo.
“Hivyo ni vyema watu wakaendelea kufahamu hilo na kuchukua tahadhari ya mazingira ili kuepuka athari mvua hizo zitakaponyesha,” alisema.
Joyce ametoa wito kwa wananchi kuendelea kufatilia vipindi na taarifa zinazotolewa na TMA ili kufahamu mabadiliko mbalimbali yanayotokea.
MAGRET BAVUMA(TUDARCo) SUPERIUS ERNEST



























