KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema ushindi katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Ushetu na Konde ni wa CCM.
Shaka aliyasema hayo, mjini Kahama mkoani Shinyanga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tathmini ya uchaguzi mdogo katika majimbo hayo utakaofanyika kesho.
“Kwa tathmini yetu CCM ina uhakika wa ushindi katika Jimbo la Konde (Mkoa wa Kaskazini Pemba), Jimbo la Ushetu (Mkoa wa Shinyanga) na kata zote tatu, kwa sababu imesimamisha wagombea wenye sifa za uongozi, wanaofahamu mahitaji ya wananchi wao, wanaokubalika na wapigakura wa rika zote.
“Zaidi, chama kimefanya kampeni za kisayansi sana zilizowafikia wapigakura wengi kuliko chama chochote zilizopokewa kwa hamasa na matumaini makubwa,” alisema.
Amesema utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika maeneo yote, kuanzia uboreshaji wa huduma za kijamii kama afya, elimu na maji safi, ni miongoni mwa mambo yaliyowapa wananchi imani kubwa kwa Chama.
Alisema tayari kata sita kati ya tisa zilizotangazwa kurudia uchaguzi, wagombea wa CCM wamepita bila ya kupingwa.
Kata ambazo CCM imepita bila ya kupingwa ni Mbuyuni (Dar es Salaam), Dogo (Manyara), Udugu (Njombe), Ndembezi (Shinyanga), Lingwa (Singida) na Kileo (Kilimanjaro).
“Hivyo ni kata tatu tu ndizo zitafanya uchaguzi siku ya tarehe 9, Oktoba, 2021 na ambazo tunauhakika wa kushinda kwa sababu tulizozieleza.
“Chama Cha Mapinduzi kina matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi katika majimbo yote ya Konde, Ushetu na kata tatu zinazorudia uchaguzi.
Amebainisha kuwa, “CCM itakuwa tayari kupokea matokeo yoyote kwani hiyo ndiyo demokrasia,” alisema.
Shaka alitoa wito kwa wana CCM na wakazi wa majimbo ya Konde, Ushetu, Kata ya Neruma Bunda mkoani Mara, Lyowa mkoani Katavi na Vumilia mkoani Tabora, kujitokeza kwa wingi na mapema asubuhi kesho, kuwachagua wagombea wanaotokana na CCM.
Aidha, aliwasihi baada ya kupiga kura warejee nyumbani kuendelea na shughuli zao wakati wakisubiri kusherehekea ushindi.
“CCM inawashukuru wanachama wake na wananchi katika maeneo yote hayo kwa namna walivyojitoa na kushiriki kampeni za wagombea wetu kwa hamasa kubwa, amani na utulivu,” alisema
Shaka alisema kampeni za uchaguzi huo zitafungwa leo, ambapo kwa upande wa Ushetu Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, ataongoza huku katika Jimbo la Konde kazi hiyo ikifanywa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla
DITOPILE ASEMA NGUVU MOJA
Akizungumza kando ya mkutano huo na waandishi wa habari, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma, Marim Ditopile, alisema kutokana na umuhimu wa uchaguzi huo amejumuika na wanaCCM kuhakikisha wagombea wa CCM wanashinda kwa kishindo.
“Tumeungana na wenzetu kuhakikisha tunapata ushindi, kazi kubwa imeshafanyika na hadi sasa kama alivyosema mwenezi (Shaka), ushindi ni uhakika kwa CCM,” alisema. Uchaguzi mdogo wa ubunge kwa upande wa Jimbo la Ushetu, unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wake, ambaye pia alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa huku kwa Jimbo la Konde unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge mteule, Mpemba Fakhi, kujiuzulu.
Katika hatua nyingine, Selina Mathew, anaripoti kuwa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata tatu na ubunge wa majimbo mawili ya Konde wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba-Zazibar na Ushetu, Mkoa wa Shinyanga unatarajiwa kufanyika kesho huku vyama vya siasa na wagombea wakikumbushwa kuzingatia sheria, kanuni za uchaguzi.
Uchaguzi huo utahusisha wapigakura 191,152 walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura na vitatumika jumla ya vituo 529 vya kupiga kura huku hati za kusafiria, leseni ya udereva na kitambulisho cha uraia zikitumika kama mbadala kwa waliopoteza kadi.
Akitoa taarifa kuhusu upigaji kura katika uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu, Semistocles Kaijage, alisema uchaguzi huo unahusisha kujaza nafasi wazi za udiwani katika kata tatu ambazo ni Vumilia iliyopo Urambo, Neruma wilayani Bunda na Lyowa Kalambo.
Alisema vyama vitano vimesimamisha wagombea katika uchaguzi na kwamba vilipata nafasi ya kufanya kampeni kwa njia mbalimbali kuanzia Septemba 20, mwaka huu hadi jana.
“Kwa ujumla kampeni katika maeneo mengi zimefanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia maadili ya uchaguzi ambayo vyama wakiwa wadau wakuu, serikali tume tulikubaliana kuyafuata.
Tume inawapongeza wadau wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla kwa kudumisha amani na utulivu.
Bila shaka hali hiyo itaendelea kuwepo hadi shughuli za uchaguzi zitakapokamilika,”alisema.