WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, ameonya na kuwataka viongozi wa kisiasa kuacha kuwatukana na kuwadhalilisha watumishi wa umma.
Mchengerwa alitoa kauli hiyo mjini Sengerema wakati akizungumza na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, madiwani na watumishi wa halmashauri za Buchosa na Sengerema.
“Sitafurahishwa kiongozi kumtukana mtumishi wa umma hadharani, wanatusaidia kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni watumishi wa umma na bila wao tutakwama hivyo tusiwadhalilishe mbele za umma na kukiwa na hoja tutafute fursa ya kuzishughulikia,” alisema Mchengerwa.
Mchengerwa aliwataka watumishi wa umma waendelee kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia taratibu na kanuni za utumishi huku akiwaonya maofisa utumishi kote nchini kutojifanya miungu watu, wapange ratiba watoke ofisini wakasikilize kero za watumishi na kuzishughulikia.
Waziri huyo wa utumishi na utawala bora, alisisitiza Rais Samia Suluhu Hassan, amepania kulinda stahiki na maslahi ya watumishi wa umma kwa kipindi kifupi amefanya kazi nzuri ya kuwapandisha madaraja watumishi 190,000 na mishahara yao.
Alisema kuelekea 2025, serikali haitaki kubaki na matatizo ya watumishi wa umma, inataka kubaki na kanzidata na misingi ya watumishi ili walioondoka watamani kurudi, hivyo waendelee kuchapa kazi na kumsaidia Rais Samia kuiinua nchi ili mwaka 2025 kazi iwe rahisi ëunachukua unawekaí na kuwa wakilegalega yote hayatafanikiwa.
Kuhusu miradi iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya hayati Dk. John Magufuli, alisema hakuna hata mmoja utakaosimama na kuonya hatataka kusikia kuna udokozi wa fedha za miradi ya maendeleo zinazopelekwa kwenye halmashauri.
Pia, alisema serikali inapeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo ya wananchi na kuitaka TAKUKURU isiwe nyuma kufuatilia matumizi ya fedha za miradi hiyo ili zionyeshe thamani yake na zilete matokeo chanya.
“Fedha hizo tunazotoa za miradi ni za wananchi, tuendelee kuwa waadilifu na haijapata kutokea fedha nyingi kiasi hiki kupelekwa kwenye halmashauri, pia mkandarasi anayepewa mradi ahakikishe ana uwezo wa kuutekeleza,” alishauri Mchengerwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Mark Makoye, alisema miradi mingi wilayani humo inasuasua na kumwomba waziri huyo awaelekeze watendaji na wataalamu kuonyesha uzalendo na uadilifu kwenye usimamizi miradi hiyo ili wananchi wanufaike.
“Ili 2025 tusiwe na kazi kubwa tunaomba miradi ikamilike kwa wakati na wananchi wanufaike, pia uwaeleze wananchi jinsi serikali itakavyowaletea maendeleo kutokana na kodi zao,” alisema Makoye.
Naye, Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu, alisema serikali itapeleka sh. bilioni moja za miradi katika vijiji vya Nyamazugo, Buzilasoga, Ngoma B na Chifunfu,pia sh. bilioni 1.5 za barabara atabadilisha matumizi sh. bilioni moja zijenge barabara za vijijini na kiasi kitakachobaki kitajenga za mitaa ya Sengerema mjini kwa kiwango cha changarawe badala ya lami.
Na BALTAZAR MASHAKA, Sengerema