WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoani Simiyu, kuhakikisha wanafuatilia na kuzuia matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na serikali kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetoa fedha kwa kila jimbo kwa ajili ya miradi ya barabara, vituo vya afya na ujenzi wa madarasa, hivyo taasisi hiyo, inatakiwa kusimamia ipasavyo ili miradi hiyo isihujumiwe.
Waziri Mchengerwa aliyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa umma katika kikao maalumu kilichofanyika mjini Bariadi na kuwataka watumishi wa umma, kuwajibika na kuzingatia waraka wa utumishi.
“Serikali imetutaka kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yetu, wakala wote wa serikali, zisimamie miradi yote na tunataka ikamilike kwa wakati, tuongeze weledi.
“Niwaombe TAKUKURU mikoani, wilayani na nchi nzima, tupambane na kuzuia matumizi mabaya ya fedha, tufuatilie matumizi ya fedha katika miradi inayotekelezwa,’’ alisema
Alisema watumishi wa umma wasipojipanga vizuri katika usimamizi wa fedha za miradi ya maendeleo, watakuwa wanawahujumu wananchi, hivyo aliiomba TAKUKURU kujipanga kusimamia fedha za miradi ya maendeleo.
Waziri huyo alisema serikali inatekeleza programu ya ujenzi wa madarasa zaidi ya 5,000 nchini, kwa hiyo aliwataka maofisa mipango, kujipanga kushirikiana na TAKUKURU kusimamia fedha ili wananchi waone kazi ya fedha zilizoletolewa na Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa aliwataka maofisa utumishi, kuendelea kuchapa kazi na kusikiliza kero za wananchi katika maeneo yao, aliwasisitiza maofisa utumishi kuendelea kubadilika kwa kutoka ofisini na kusikiliza kero za watumishi na wanachi.
“Pokeeni malalamiko yao, andaeni utaratibu wa kukutana na watumishi, zipo kero ambazo tungeweza kuzitatua bila bajeti ya serikali, tuendelee kubadilika katika utendaji wa kazi katika maeneo yetu, tuzingatie waraka na kanuni za utumishi wa umma katika utendaji wa kazi,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Tuzingatie waraka wa mavazi katika maeneo yetu, baadhi ya watumishi kutumia zaidi simu (mtandao ya kijamii) badala ya kusikiliza kero za wananchi, watumishi kote nchini, tuwajibike kujenga imani na matumani kwa wananchi.”
Aliwataka watumishi kujikita katika misingi ya umma na kwamba, wana jukumu la kubeba kero za wananchi pia watambue jukumu lao na waajiri wao ni wananchi, alisisitiza kuwatendea haki wananchi katika maeneo yao, kufanya kazi kwa weledi, kujitoa, pia maofisa mipango kujipanga kuongeza mapato Mkoa wa Simiyu.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, aliiomba serikali kuendelea kutoa ajira hususan kipaumbele kwa Mkoa wa Simiyu, ambapo pia nyingi za umma bado ziko kwenye majengo ya kupangisha ambayo ni gharama kwa serikali.
Alisema tangu Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III) uanze katika mkoa huo, umeweza kuzinufaisha kaya 45,000 na sh. bilioni 38.86 zimetumika katika mpango huo ambao umeinua vipato na maisha ya walengwa.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi



























