WAKULIMA wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi, Mwambao kinachohudumia Wilaya za Kilwa na Lindi, wamekataa kuuza korosho zao mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania, Brigedia Jenerali Mstaafu, Aloyce Mwanjile.
Zaidi ya tani 1,895 na kilo 597, zimekataliwa na bei ya juu ilikuwa sh. 2,275 na bei ya chini sh. 2,010.
Akizungumza katika mnada huo wa kwanza kwa chama cha Mwamboa, Mwanjile amewaomba wakulima kuwa watulivu kwa kuwa serikali yao, imelipokea suala hilo na litafanyiwa kazi mara moja.
Mwanjile amesema mnada huwa wazi, ndiyo maana wakulima wameamua kuuza au kutouza.
“Kama kiongozi wenu, nimelichukua na litafanyiwa kazi, lakini niwatoe hofu serikali yenu imelipokea, changamoto yenu ya ucheleweshaji wa pembejeo kwa mwakani, italetwa mara moja,” alisema Mwanjile .
Aliongeza kuwa:”Niwaombe mwendelee kulinda ubora wa korosho katika maghala yenu, viongozi wote wa ushirika kuweni waadilifu katika kuwapa fedha wakulima kwa wakati pindi korosho hizo zinaponunuliwa katika minada yenu.”
Mwanjile amesema wakulima ndio wenye maamuzi katika kuuza korosho zao, aliwatoa hofu kuwa, kila mkulima atauza na atapata fedha yake kwa wakati kwani, serikali kwa sasa ipo macho katika kuhakikisha mkulima anapeleka korosho zake katika stakabadhi ghalani.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Frances Alfred, aliwasihi vyama vya ushirika kuwa waadilifu na waaminifu na uwajibikaji katika kuwatumikia wakulima kwa kuwapa fedha zao kwa wakati.
“Nawaomba niwakumbushe wakulima nchi nzima kuangalia akaunti zenu vizuri ili mnapoingiziwa fedha za korosho, iwe rahisi kuziona na kujua, maana wakulima wengi akaunti zao zimelala sana, ndiyo maana hampati fedha zenu kwa wakati, hivyo muweke akaunti vizuri, muwe mnazitumia mara kwa mara,” alisema Alfred.
Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao, Ismail Nalinga, aliwaomba wakulima kuwa watulivu na suala hilo la kukataa kuuza korosho zao, litashughulikiwa na watafanya mnada mwingine ndani ya wiki ijayo.
“Kama mwenyekiti nimelipokea na mimi ni mkulima mwenzenu, kama mmekataa hili, basi wiki ijayo tutafanya mnada mwingine tujue kama bei itapanda au itakuwa vilevile,” alisema Nalinga.
Kwa upande wao, baadhi ya wakulima, walisema wamekataa kuuza bei hiyo na kuomba serikali kusikia kilio chao.
Mkulima wa Kata ya Nachunyu, Halmashauri ya Mtama, John James, alisema wakulima wa Wilaya ya Lindi, wamekataa kuuza korosho kwa bei hiyo na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan, aweze kusikia kilio chao.
“Wanunuzi wanatuonea, bei wanayokuja nayo ni ndogo sana, tunakusii mama yetu Samia,” alisema James.
Naye Asha Hussein, ambaye ni mkulima wa Amcos Natam, alisema walipeleka korosho zao, lakini wanunuzi hawataki wakulima wapate fedha nzuri, akawaomba viongozi wafuatilie suala hilo.
Na Sophia Nyalusi, Lindi



























