SERIKALI imeanisha maeneo saba ambayo itayawekea msimamo katika mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN), kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.
Hayo yalibainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, wakati akitoa tamko kuhusu msimamo wa Tanzania katika mkutano huo utakaofanyika jijini Glasgow nchini Scotland, Oktoba 31 hadi Novemba 12 mwaka huu.
Amesema Tanzania itashiriki kikamilifu katika majadiliano yenye maslahi mapana ya nchi na kuweka msimamo kwa kuwa athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa sasa ni moja ya changamoto zinazolikabili taifa kiuchumi, kijamii na ustawi wa watu.
Amesema msimamo wa kwanza utahusu eneo la rasilimali fedha ambapo kwa mujibu wa mkataba huo, nchi zilizoendelea ziliahidi kutoa kiasi cha fedha dola bilioni milioni 100 kila mwaka ifikapo 2025, kuweka mipango ya kimkakati kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Msimamo wa Tanzania katika suala hili ni kuzitaka nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao wa ahadi ya kutoa fedha hizi kama ilivyokubaliwa,” amesema.
Amesema msimamo mwingine wa nchi ni katika suala la kujenga uwezo kwa kuzitaka nchi zilizoendelea pamoja na mashirika ya kimataifa, kutilia mkazo suala la kujenga uwezo wa nchi zinazoendelea ili zitoe mchango kupunguza uzalishaji wa gesi joto duniani.
Katika eneo la kilimo na mabadiliko ya tabianchi, alisema msimamo wa nchi ni kwamba sekta hiyo isijumuishwe katika sekta zinazotakiwa kuunguza gesi joto kwa kuwa kinaathirika na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha, amesema katika uendeleaji na usambazaji teknolojia, alisema msimamo wa Tanzania ni kwamba nchi zilizoendelea zihakikishe zinapatiwa teknolojia hizo kwa gharama nafuu na kwa uwazi.
Pia, amebainisha kuwa suala la mchango wa taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi alisema msimamo ni kuwa mkutano huo ufikie maamuzi yatakayowezesha upatikanaji wa fedha za kuwezesha nchi zinazoendelea kutekeleza michango yao na mapitio yafanyike kila baada ya miaka mitano.
Vilevile, amesema kwa eneo la upunguzaji gesi joto kwa kutumia biashara, alisema msimamo ni kuwa nchi inazouza ziada isijumuishe kiwango kilichouzwa katika orodha yake ili kusitokee kuhesabiwa mara mbili kwa nchi iliyonunua ziada.
Ameongeza kuwa katika jinsia na mabadiliko ya tabia nchi, msimamo wa nchi unahimiza utekelezaji wa programu ya miaka mitano ili kuwepo uwezeshaji wa wanawake ambao utaleta mafanikio yenye ufanisi mkubwa katika nyanja za kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi na kupunguza gesi joto.
Waziri Jafo amesema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni muhimu kwa vile utawezesha nchi kufaidika na fursa mbalimbali kama upatikanaji wa fedha na teknolojia zitakazosaidia serikali kukubaliana na athari hizo.
“Ushiriki wa nchi yetu katika mkutano wa COP 26 unatarajiwa kuleta faida kwa nchi, kupata rasilimali fedha na utaalamu utakaowezesha utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali ya kupunguza na kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Na SELINA MATHEW, DODOMA



























