MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), iko mbioni kufungua ofisi ndogo katika balozi ambazo nchi zake zinatumia Bandari za Tanzania kushusha shehena.
Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa Bandari Mkoa wa Tanga, Donard Ngaile wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alipotembelea bandarini hapo kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa Bandari hiyo.
“Lengo la kuweka ofisi katika balozi hizo, ni kuhakikisha tunapanua wigo wa utafutaji wa masoko na ushawishi kwa nchi zinazotumia Bandari za Tanzania,” amesema.
Awali, Profesa Mbarawa baada ya kukagua mradi huo alitoa agizo kwa Mamlaka za Bandari Tanzania kuhakikisha wanawekeza nguvu katika utafutaji wa masoko kwa watumiaji wa Bandari za Tanzania.
“Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miradi ya bandari zetu hivyo niwatake na ninyi kuhakikisha mnapambana kutafuta masoko kwa wateja wa nchi wanazotumia bandari zetu ili kuleta tija katika kuongeza pato la taifa,” amesema Waziri Mbarawa.
Mradi wa upanuzi wa lango la kuingilia meli katika Bandari ya Tanga Umegharimu kiasi cha Sh bilioni 256 na unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka 2022.
Susan Uhinga, Tanga.