CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kitasimamia matumizi ya sh. trilioni 1.3 za mkopo wa masharti nafuu zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF), ambazo zinakwenda kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuhakikisha hazitafunwi na mbadhirifu yeyote, na atakayebainika atachukuliwa hatua kali.
Pia, kimeagiza kamati za siasa kuanzia ngazi ya mkoa hadi kata kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, ili matokeo chanya yapatikane, kwani fedha hizo siyo sadaka, hivyo matumizi yake yanapaswa kuheshimika.
Akizungumza jijini Dodoma katika ukumbi wa White House uliopo katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema chama kitahakikisha fedha hizo zinakwenda kutekeleza miradi iliyokusudiwa kwa wananchi.
“CCM ndicho chama kilichoshika hatamu ya uongozi wa nchi, hivyo kinawahakikishia Watanzania, fedha hizi hazitafunwi na mchwa na atakayethibitika kuhusika na ukwapuzi wa aina yoyote Chama Cha Mapinduzi hakitasita kuielekeza serikali kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Katika hili tunazielekeza wizara zote zitakazonufaika na fedha hizi kujipanga vizuri katika usimamizi kama alivyoelekeza Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Samia Suluhu Hassan, kwasababu fedha hizi za mkopo kutoka IMF siyo za sadaka, hivyo ziheshimiwe.”
Shaka alisema CCM inawataka viongozi na watendaji wenye dhamana kuanzia serikali kuu hadi halmashauri za wilaya, wahakikishe fedha hizo zinakwenda kutekeleza miradi iliyokusudiwa, ili kuleta matokeo yaliyolengwa kwa ustawi wa wananchi.
“Fedha hizi na zingine zinazotolewa na serikali kwenda katika miradi mbalimbali ya maendeleo, CCM haitakubali kuona zikitumiwa visivyo na kukibebesha lawama chama ambacho kimepewa dhamana na wananchi ya kuunda na kuongoza serikali,” alieleza.
Alieleza kuwa CCM inampongeza Rais Samia na serikali anayoiongoza kwa kufanikisha majadiliano yaliyosaidia kupatikana fedha hizo kwa matumizi ya mazingira yaliyoko nchini, badala ya kubanwa katika maeneo ya ununuzi wa chanjo za Uviko- 19 pekee.
Alibainisha kuwa Rais Samia amethibitisha uwezo mkubwa alionao katika mawanda ya uongozi kwa kutetea na kulinda maslahi ya nchi.
“Chama kinatoa wito kwa viongozi wa CCM ngazi zote ambao miradi mbalimbali ya maendeleo inatekelezwa katika maeneo yao, kuisimamia na kuifuatilia kwa karibu, kwani huo ni utekelezaji wa ilani yetu ya uchaguzi.
“Lengo ni kupata mafanikio yaliyokusudiwa na kuendelea kujenga imani kwa wananchi waliotupa ridhaa ya kutoa uongozi wa nchi yetu, huo ni wajibu wetu wa msingi kwa mujibu wa ibara ya 251(d) ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025,” alisisitiza Shaka.
MAFANIKIO YA RAIS SAMIA
Aidha, Shaka alisema CCM inatoa pongezi za dhati kwa Rais Samia kwa kuwa ameonyesha ushupavu, uzalendo na kuwa mwanamageuzi kwa kuendelea kulinda tunu za taifa na kusimamia msingi mkuu wa kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Alieleza kuwa Rais Samia ameendelea kulinda na kuimarisha utawala wa sheria, demokrasia ya vyama vingi, usawa, haki za binadamu, nchi kutofungamana na dini yoyote, kupambana dhidi ya unyanyasaji, ubaguzi na udhalilishaji wa aina zote.
“Rais Samia ameendelea kuimarisha utumishi wa umma kwa kuuwekea mazingira mazuri kimaslahi kwa kupunguza kodi katika mishahara (PAYE) kutoka asilimia tisa hadi nane na kufuta tozo ya asilimia sita ya thamani ya mikopo elimu ya juu.
“Pia, amepandisha madaraja kwa mujibu wa sheria watumishi 180,000 wenye sifa za weledi, nidhamu, uadilifu, ubunifu, bidii na maarifa katika kazi,” alifafanua.
Shaka alisema Rais Samia ameendelea kudhibiti na kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, utakatishaji fedha, uhujumu uchumi na dawa za kulevya.
Pia, alisema katika kujenga na kukuza uchumi wa kisasa serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki, wezeshi na yanayotabirika, ili kuchochea ukuaji wa sekta binafsi, kuvutia uwekezaji, kuzalisha ajira na kuongeza wigo wa kodi kwa serikali.
Alieleza kuwa Rais Samia ameshatoa mweleko wa kujenga Tanzania bora zaidi ambayo kila mwananchi ataendelea kuifurahia na kujivunia zaidi kwa kuwa Watanzania wamejaliwa kuwepo katika nchi nzuri.
MATOKEO UCHAGUZI MDOGO
Akizungumzia matokeo ya uchaguzi mdogo katika majimbo ya Ushetu na Konde, Shaka alisema CCM inawashukuru wananchi wa Jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga kwa kumchagua aliyekuwa mgombea wa CCM, Emanuel Cherehani, kwa kura 103,357 sawa na asilimia 96% dhidi ya kura 3,588 za mgombea wa Chama Cha ACT Wazalendo.
Kadhalika, alisema CCM inawashukuru wananchi wa kata tatu za Tanzania bara ambazo ni Neruma (Bunda, Mara), Lyowa (Kalambo, Katavi) na Vumilia (Urambo, Tabora) kwa kuipa ushindi mkubwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika Oktoba 9,2021.
Pia, alisema CCM inatoa pongezi kwa ACT Wazalendo kwa ushindi katika Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
“Hii ndiyo maana halisi ya dhana ya siasa safi na demokrasia ya kweli ambayo Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Samia Suluhu Hassan aliahidi kuheshimu na kulinda katika uongozi wake.
“Tunawashukuru wanachama na wananchi wa Jimbo la Konde kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi japo kura hazikutosha, tunaamini maneno ya wahenga, tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuleta maendeleo katika Jimbo la Konde,” alisisitiza.
Alisema kumalizika kwa uchaguzi huo mdogo kwa amani na utulivu ni jambo la kujivunia, kwani kunaendelea kuimarisha umoja na mshikamano.
MAONO YA RAIS SAMIA
Shaka alisema CCM inaendelea kuwaomba Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwani ana maono makubwa kwa dhamira ya kuijenga Tanzania yenye maendeleo na neema zaidi.
“Hili linadhihirika kwa namna anavyoendeleza na kuimarisha diplomasia ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Anavyoendeleza kwa kasi miradi mbalimbali ya miundombinu ya kimkakati kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), uimarishaji wa Shirika la Ndege (ATC) na ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere.
“Ujenzi wa meli katika maziwa makuu na Bahari ya Hindi, uimarishaji wa huduma za msingi za kijamii kama maji safi na elimu katika namna ambayo itarejesha fedha katika mzunguko na mifuko ya wananchi wachapakazi.
Oktoba 10, mwaka huu, Rais Samia alifanya uzinduzi wa kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 ambayo inagharimu sh. trilioni 1.3, ikiwa ni msaada na mkopo wa masharti nafuu IMF.
Katika fedha hizo, serikali inatarajia kujenga madarasa, kununua magari ya wagonjwa, ununuzi wa mashine za kisasa za matibabu, magari ya wagonjwa, mitungi ya kuzalisha hewa safi kwa wagonjwa, kununua chanjo ya Uviko-19, kujenga vyuo vya ufundi stadi na kuwezesha kaya masikini.
Na MUSSA YUSUPH, DODOMA



























