WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, amesema sh. bilioni 90.2 walizopatiwa kutoka katika fungu la fedha za mapambano ya Uviko 19, la Tsh. trilioni 1.3 za Shirika la Fedha Duniani (IMF), watazitumia kununua vifaa vya kupimia ugonjwa huo na kuboresha miundombinu maeneo ya hifadhi.
Aidha, amesema watatumia fedha hizo kugharamia mafunzo kwa wadau wa utalii, wakiwemo madereva wa magari ya watalii, waongozaji, wabeba mizigo na wahudumu wa hoteli za kitalii.
Dk. Ndumbaro aliyasema hayo jijini Arusha, wakati wa mkutano wa wizara hiyo na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania ( TPSF), uliolenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokabili sekta ya utalii, hususan kipindi cha ugonjwa wa Uviko 19 na kufafanua kuwa vifaa vitakavyonunuliwa vya kupimia ugonjwa wa huo vitasambazwa maeneo yote ya vivutio vya utalii.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, wakiwemo kutoka Chama cha Waongoza Watalii (TATO), Baraza la Biashara la Taifa, TPSF, Chama cha Waongoza Watalii, Chama cha wadau wa Utalii wa Utamaduni (TACTO) na Chama cha Mahotelia Tanzania (HAT)
Dk. Ndumbaro alibainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha hizo ili kuinyanyua sekta ya utalii nchini kutokana na janga la Uviko 19, ambalo limeiacha sekta hiyo katika hali tete, huku watalii wakisitisha safari za kuingia nchini.
Alifafanua kuwa vifaa vitakavyonunuliwa vya kupimia Uviko 19 vitasambazwa maeneo yote ya vivutio vya utalii ili watalii watakapopimwa wapewe majibu yao huko hukom, tofauti na ilivyo sasa.
“Tumedhamiria kuondoa usumbufu kwa watalii kwa kuhakikisha kila hifadhi inatoa huduma hizo kwa haraka ili wasikae kusubiri matokeo kwa muda mrefu, “alisisitiza.
Kuhusu miundombinu, Dk. Ndumbaro aliweka wazi kuwa ujio wa fedha hizo utasaidia kufungua hifadhi kama ya Taifa ya Nyerere, ambayo ina barabara nyingi, lakini hazipitiki, zitasaidia kuziboresha na kupitika mwaka mzima.
Mbali na hilo, Dk. Ndumbaro alisema barabara zitaboreshwa na nyingine zitafunguliwa katika maeneo ya hifadhi ambayo hayana miundombinu hiyo ili yafikike kwa urahisi.
“Barabara ikiwa nzuri na wewe una hoteli yako ipo ndani sana, watalii watakuja kulala katika hoteli yako kwa sababu kuna barabara nzuri. Hivyo fedha hizi zinakwenda kufanya kazi hiyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula, alimshukuru Rais Samia kwa kujitoa kuisaidia sekta ya utalii nchini.
”Tunaomba salamu zifike kwa Rais Samia kwa juhudi za kuendeleza utalii kwa kututafutia fedha kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF). Tumemwona anavyoipambania sekta ya utalii kupitia kipindi chake maarufu alichokiasisi cha Royal Tour, ambacho kimeongeza ujasiri kwa wawekezaji wa sekta ya utalii nchini. Tunampongeza sana rais wetu,” alisema.
Angelina aliwataka wadau wa utalii nchini kuungana kwa kuwa kitu kimoja ili wanapotaka kuwasilisha agenda zao serikalini zikubaliwe na kufanyiwa kazi.
Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara, Dk. Godwill Wanga, aliiomba wizara kupitia fedha zilizotolewa na IMF za kupambana na UVIKO 19, zisaidie kuboresha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege, kwa lengo la kuwavutia watalii wanapotembelea vivutio vya utalii na wafike kwa urahisi.
Pia, aliiomba wizara hiyo kupitia fedha hizo, kusaidia kutoa mafunzo kwa wadau wa utali ili wawe wanatoa huduma bora kwa watalii. Ombi hilo lilikubaliwa na kuahidiwa kuanza kufanyiwa kazi.
Na MWANDISHI WETU, ARUSHA



























