WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, amesema wizara hiyo, imepokea sh. bilioni 90.2 zitakazotumika kutekeleza miradi mitano na shughuli 23, ikiwa ni sehemu ya fedha za mkopo nafuu wa sh. trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Amesema miongoni mwa miradi hiyo, mitano ni kuziboresha taasisi za wizara hiyo ili zitekeleze majukumu yake kwa kuimarisha miundombinu na kununua vifaa mbalimbali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Dk. Ndumbaro alizitaja taasisi hizo ni Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Taasisi ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Hifadhi ya Ngorongoro.
Alifafanua katika mradi huo wa kwanza kutakuwa na shughuli tisa, ambazo ni ujenzi wa barabara kilomita 4,881 zitakazotumia sh. bilioni 23 ya fedha hizo na kwamba hifadhi tisa zitanufaika.
“Fedha hizi zinakwenda kuboresha miundombinu iliyoharibika wakati wa ugonjwa wa virusi vya corona hifadhi za Ifakara, Serengeti, Mkomazi, Talangile, Nyerere, Kilimanjaro, Saadan, Gombe, Ngorongoro na maeneo ya hifadhi ya misitu 10,” alisema.
Aliyataja maeneo mengine ni kununua mifumo ya kielektroniki kufuatilia mitambo itakayonunuliwa, kujenga na kukarabati viwanja vya ndege vinane, mageti matano, ununuzi wa boti ya kioo na ukarabati wa miundombinu ya utalii yakiwemo mapori ya akiba 11 na tengefu sita.
Alisema miradi mingine ni unuzi wa mtambo wa kuchimbia visima, kuimarisha na kuboresha huduma za utalii, kuboresha maeneo ya malazi ya watalii, ununuzi wa magari, kuimarisha masoko na kutangaza utalii.
Dk. Ndumbaro alifafanua, kupitia fedha hizo vituo saba vya urithi wa kiutamaduni vitaboreshwa, kituo cha kutolea taarifa za utalii kitajengwa, vituo vyote vya utalii vitatembelewa na kutangazwa ikiwa ni hatua za kuendeleza Royal Tour iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisisitiza fedha hizo pia, zitawezesha kufanyika kwa maonyesho makubwa ya utalii mara kwa mwaka nchini, kuimarisha huduma za watalii, kutoa elimu ya utalii kwa wadau na kusambaza vifaa vya kujikinga na Uviko-19.
Kuhusu mwelekeo wa utalii nchini, Dk. Ndumbaro alisema tangu Tanzania ipate chanjo, kumekuwa na mwamko mzuri wa watalii kutembelea nchini.
Hata hivyo, alieleza katika kipindi cha miezi iliyobaki mwaka huu, ndege tatu za watalii zinatarajiwa kutua nchini kuleta watalii kutoka mataifa mbalimbali.
Alisema wakati wa janga la Uviko-19, Tanzania iliingiza watalii 620,000 kutoka nje, lakini tangu kuanza kwa chanjo, mwaka huu jumla ya watalii 623,800 wameingia nchini na bado mwaka haujakwisha.
Na JUMA ISSIHAKA



























