WANANCHI wa Wilaya ya Igunga, Mkoani Tabora wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kujali afya na maendeleo ya wananchi kwa kuweka mazingira rafiki ya kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO19.
Pongezi hizo walizitoa walipozungumza na UhuruOnline kwa nyakati tofauti.
Mkazi wa Jimbo la Manonga, Wilayani humo, Justin Shayo, amesema kitendo cha kutenga fedha za ujenzi vyumba vya madarasa kitasaidia kuweka uwiano sahihi wa wanafunzi darasani, ambapo ni njia mojawapo ya kupambana na ugonjwa huo.
“Ni jambo kubwa ambalo linapaswa kupongezwa kwa serikali ya awamu ya sita, kwa kutambua shida na mahitaji ya wananchi wake kwa kuwa miradi hiyo inagusa moja kwa moja maisha ya watu waliopo vijijini na mijini,” alifafanua.
Aidha, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Dk. Amon Hysa, amepongeza jitihada za serikali kuona umuhimu wa kupambana na ugonjwa wa UVIKO19 katika kuboresha huduma za afya na utoaji wa chanjo.
Alisema kitendo cha kutolewa fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa wakati mmoja halijawahi kutokea, hivyo wananchi wanatakiwa kuunga mkono jitihada hizo na hatua za kukabiliana na Uviko-19.
Mbunge wa Jimbo la Igunga, Mkoani Tabora, Nicholaus Ngassa, alisema uamuzi wa Rais Samia kutoa fedha za Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini ni jambo la kuungwa mkono.
Alisema miradi iliyotengewa fedha ni ujenzi wa vyumba vya madarasa 92 vitakavyogharimu sh. bilioni 1.8, hivyo kuondoa upungufu wa madarasa ya shule za sekondari Wilaya ya Igunga.
Ngassa alisema fedha nyingine sh. milioni 160 za ujenzi wa vyumba vya madarasa manane shikizi ambayo ni ya maandalizi ya wanafunzi wa elimu msingi.
Alisema kwa upande wa afya zimetengwa sh. milioni 100 za ujenzi wa chumba cha huduma za wagonjwa mahututi (ICU) katika Hositali ya Wilaya ya Igunga.
Alieleza ili kukuza ustawi wa jamii na maendeleo ya watu, serikali imepanga kutekeleza ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi wa afya ambazo zitagharimu sh. milioni 90.
Na ODACE RWIMO, IGUNGA



























