WANANCHI zaidi ya 300 kutoka katika kijiji cha Kemgesi Kata ya Nyamatare Wilayani Serengeti Mkoani Mara wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro wa ardhi katika bonde La Mwibara kati ya kijiji hicho na vijiji vya Masinki, Maburi pamoja na Ring’wani.
Wakiongeongea katika Mkutano wa kijiji wananchi hao wamesema wamekua wakilitumia eneo hilo lenye hekari zaidi ya 800 kwa shughuli za kilimo na ufugaji lakini tangu kuibuka kwa mgogoro huo wa mpaka wameathirika pakubwa na hivyo kuiomba serikali kupitia Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi kusikia kilio chao.
Magreth Kichemli, Charles Chacha pamoja na Wansore Machota ni miongoni mwa wakazi ambao wamesema hivi sasa maisha yao yako hatari kutokana na mgogoro huo ikiwa ni pamoja na kushindwa kufanya maandalizi ya shughuli za kilimo katika msimu huu.
Chacha Mahemba ni Mwenyekiti wa Kijiji hicho na Gechera Edwin ni Diwani wa kata ya Nyamatare kwa upande wao wamewaomba viongozi wenye dhamana kufika katika kijiji hicho ili kuwasaidia wananchi hao ambao Kwa sasa ni waathirika wakubwa wa mgogoro huo kutoka na kutegemea eneo hilo ili kukidhi mahitaji katika maisha yao ya kila siku.
Na Emmanuel Chibasa- Mara



























