YANGA ambao ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imeingia kambini kwa ajili ya kujiandaa kuikabili Azam FC katika mchezo uliopangwa kufanyika Oktoba 30, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Timu hiyo yenye maskani yake Jangwani ambayo inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi tisa, itakuwa mwenyeji wa mchezo huo namba 31.
Huo utakuwa mchezo wa nne tangu michuano ya ligi kuu imeanza kutimua vumbi Septemba 27, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze, alisema leo wanaingia kambini ambapo wataanza mazoezi rasmi ya kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Azam ambao wamepania kuendeleza makali yao katika ligi.
“Tumeanza na pointi tatu tatu ni hakuna kupumzika hadi tutakapofikisha pointi 75 ambazo zitatupa ubingwa, tutapambana kufikia malengo yetu kikubwa ni ushirikiano kati yetu,” alisema Kaze.
Alisema wameanza mazoezi mapema ili kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na rekodi ya klabu hizo katika misimu ya karibuni.
Kutokana na mchezo huo kutarajiwa kujaa upinzani, Kaze aliwaomba mashabiki wa Yanga kuendelea kuwapa sapoti katika mechi hiyo na nyingine zilizoko mbele yao, ili wafikie malengo ya kuzoa ushindi.
Yanga imepania kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kushindwa kutamba misimu minne mfululizo, huku Simba iking’ara katika vipindi hivyo.
Katika michezo mitatu ambayo Yanga imeshinda, hadi sasa imetupia wavuni jumla ya mabao manne baada ya kuinyoa KMC mabao 2-0, ilishinda 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na kuikaribisha kwa kichapo katika ligi kuu timu ngeni ya Geita Gold baada ya kuilamba bao 1-0.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zacharia Thabit ‘Zaka Zakazi’, alisema kwa sasa wana kibarua kigumu dhidi ya timu ya Pyramids ya Misri kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo baada ya kumaliza majukumu hayo ya kimataifa watazungumzia mechi hiyo ya ligi kuu Bara.
“Tuna majukumu ya mechi ya kimataifa tutakuwa na nafasi nzuri baada ya kumaliza kucheza dhidi ya Pyramids,” alisema.
Wawakilishi hao wa Tanzania katika michuano hiyo ya Shirikisho Afrika waliondoka nchini juzi kuifuata Pyramids itakayocheza nayo kesho.
Mchezo wa kwanza uliopigwa Dar es Salaam, timu hizo zilimaliza dakika 90 bila kufungana.
Na ELIZABETH JOHN