SERIKALI mkoani Mwanza, imepokea sh. bilioni 20.2 za ujenzi wa miundombinu ya elimu, imesisitiza kabla ya kuanza ujenzi, nyaraka za manunuzi na malighafi zitakazotumika, zikaguliwe ili kuepuka kuibiwa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoani hapa.
Alisema hatakubali fedha hizo kuibiwa kwa sababu ujenzi ni hesabu, hivyo kabla ya kujenga, malighafi zote na nyaraka za manunuzi, zitakaguliwa kwa lengo la kujiridhisha.
“Nikiri wazi kuwa, fedha tulizopewa zaidi ya sh. bilioni 22 ni historia ya nchi tangu tumepata uhuru, zinakwenda katika maendeleo. “Bajeti ni kitu kingine na kutekeleza ni jambo jingine, maelekezo ya kuzisimamia fedha hizo ni kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,”alisema.
Mhandisi Gabriel alimhakikishia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo kuwa, asiwe na shaka katika utekelezaji wa ilani na miradi ya maendeleo.
Alizitahadharisha kamati za usimamizi na ujenzi kila wilaya kuwa, kuna haja ya kuzisimamia fedha hizo kwa Chama na Serikali, ambapo vitaundwa vikundi vya vijana kila wilaya kwa kazi ya ujenzi na wasiotaka watanyang’anywa kazi na kupewa wengine.
Mkuu huyo wa mkoa, alisema kila wilaya imetengewa sh. milioni 150 za kuchimba msingi na fedha itakayobaki, itasaidia kutekeleza majukumu mengine, kutakuwa na mikataba midogo kila hatua ya ujenzi.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Diallo akifungua mkutano huo wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa, alisema wakuu wa mikoa wamebebeshwa mzigo wa usimamizi wa fedha za ujenzi wa madarasa.
“Kilio cha RC kujenga madarasa, sasa hofu yake imeisha, kilichobaki ni kusimamia fedha zilizotolewa na serikali,” alieleza.
Na BALTAZAR MASHAKA,Mwanza



























