MVUA iliyoambatana na upepo imeezua nyumba zaidi ya 50 zilizopo kata ya Ngulyati iliyopo wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Lupakisyo Kapange, baada ya kufika katika eneo la tukio huku akiwataka waathirika wa tukio hilo kutotumia nyumba zilizoezuliwa badala yake wajihifadhi kwa majirani wakati serikali inafanya utaratibu wa kuona namna ya kuwasaidia.
“Kitongoji cha kadoto nyumba 22 zimeezuliwa na kitongoji cha Ngulyati nyumba 30, niwaombe wananchi wasitumie nyumba hizi kwasasa wajihifadhi kwa majirani hata katika shule zetu za msingi na sekondari zinaweza kuwahifadhi kwa muda wakati serikali ikifanya utaratibu …tunachoshukuru Mungu hakuna maafa kwa binadamu ” amesema DC Kapange
Mvua iliyoambatana na upepo imenyesha jana majira ya saa kumi jioni na kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu huyo hakuna vifo wala majeruhi.
Baadhi ya wananchi waliokumbwa na changamoto hiyo wamesema baadhi ya mabati yamejikunja mengine yamepeperushwa na upepo huku nyumba nyingine ziking’oka paa lote.
” Nilikuwa shambani ghafla hali ya hewa ikabadilika ikabidi nirudi nyumbani watoto walikuwa nyumba ya jirani mara upepo ukaanza ghafla paa likang’ oka lote” amesema Agnes Malongo Mhanga wa tukio hilo mkazi wa Ngulyati.
Na Anita Balingilaki ,Bariadi





























