SUDAN imeingia katika historia nyingine baada ya kudaiwa kuwepo kwa mapinduzi ya jeshi dhidi ya serikali ya mpito nchini humo, ambapo Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abdallah Hamdok, kuwekwa kizuizini nyumbani kwake.
Mbali na Waziri Mkuu kuwekwa kizuizini nyumbani kwake, pia mawaziri wengine katika serikali ya mpito nao wamekamatwa na kundi hilo la wanajeshi.
Taarifa mbalimbali zilizokuwa zinatolewa na vyombo mbalimbali vya habari mjini humo, vilisema mapinduzi hayo yalifanyika leo asubuhi wakati wanajeshi hao walipokwenda katika nyumba za viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Ilisema baadhi ya vikosi vya jeshi vimewatia mbaroni wawakilishi wa kiraia wa baraza la uongozi wa mpito la Sudan na mawaziri kadhaa wa serikali ya mpito ya nchi hiyo.
Televisheni ya al Hadath ya Sudan imesema Hamdok amewekwa chini ya kifungo cha nyumbani na kuwekwa chini ya ulinzi baada ya vikosi vya jeshi visivyojulikana kuizingira nyumba yake huku picha kadhaa zikiwaonyesha wanajeshi wakiwa katika sare nje ya makazi ya Waziri Mkuu.
Wakati huo huo uwanja wa ndege wa Khartoum umezingirwa na huduma za intaneti zimekatwa huku Jumuiya ya Wataalamu ya Sudan (The Sudanes Professionals Association) ikiwataka wananchi kuandamana mitaani kuzima jaribio hilo la mapinduzi.
Jumuiya hiyo imesema inawahimiza wananchi kuandamana kwa wingi mitaani, waweke vizuizi barabarani na kufanya mgomo wa kutokwenda kazini ili kukabiliana na jaribio hilo la mapinduzi.
Katika upande mwingine, Chama cha Kikomonisti cha Sudan kimesema kuwa hayo ni mapinduzi kamili ya kijeshi yaliyochochewa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan, ambaye ni Mkuu wa Baraza la utawala la Sudan. PARS TODAY