SERIKALI ya Wilaya ya Malinyi, Mkoa wa Morogoro, imesema imeandaa mkakati wa kutokomeza mila potofu zinaendelezwa na baadhi ya wafugaji kuozesha watoto wadogo wa kike kuanzia umri wa miaka minane hadi 15 maarufu kama ‘Chagulaga’.
Akizungumza katika tamasha la vijana balehe lilofanyika Tarafa ya Mtimbira, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mathayo Maselle, alisema hawatavumilia kuona jamii hiyo ikiendeleza mila za chagulaga wakati wakielewa desturi hiyo inamnyima mtoto haki yake ya msingi.
Katika hotuba yake iliyosomwa na Ofisa Tarafa wa Malinyi, Rehema Hassan, Mkuu wa Wilaya huyo, alisema serikali itawachukulia hatua za kisheria wazazi wanoozesha watoto wao na kutoa elimu kwa wafugaji kuacha vitendo hivyo.
“Tunajua kuwa kila kabila lina mila zake, lakini katika hili la kumnyima mtoto wa kike haki yake ya msingi ya kielimu, hatutaweza kukubali, kwani tutakuwa tunamangamiza taifa kwa kuendekeza mila potofu,” alisisitiza.
Alilipongeza shirika la Solidarmed Malinyi kwa kuwa mdau namba moja katika sekta ya afya na serikali kwa kushirikiana na halmashauri wataendeleza ushirikiano huo.
Awali, Mratibu wa Afya ya Jamii wa shirika hilo, Malinyi Makwisa, alisema mila na desturi potofu katika kupambana na masuala ya afya ya uzazi pamoja na ukatili wa kijinsia.
Gissela aliiomba serikali kudhibiti mila potofu huku akitaja changamoto nyingine ya kuibuka wimbi la ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto kubakwa na kulawitiwa.
Alisema tamasha la mwaka huu lililenga kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana balehe kuanzia miaka 10 hadi 24 na mafunzo ya afya ya uzazi yalitolewa katika vijiji 14.
Alibainisha kuwa mpaka sasa mafunzo ya afya ya uzazi kwa makundi mbalimbali yamefanyika na kuanzishwa klabu za afya ya uzazi shuleni, vituo vya kutolea huduma, utayarishaji na usambazaji wa vipeperushi vya kutolea elimu ya afya ya uzazi, msaada wa vitendea kazi na uanzishwaji wa huduma rafiki za afya ya uzazi.
Na Igamba Libonge, Malinyi



























