WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, amesema Tanzania inazidi kupaa katika sekta ya utalii, baada ya mkutano wa kimataifa wa utalii na masoko kupangwa kufanyika Novemba, mwaka huu, Jijini Arusha.
Dk. Ndumbaro amesema hatua hiyo ni mwendeezo wa kampeni ya kipindi cha Royal Tour, kilichobuniwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kueleza kuwa kampeni ya Royal Tour, haitapowa kwa kuwa wizara yake imejipanga kutekeleza mikakati kabambe ya kutangaza sekta ya utalii katika ngazi ya kitaifa na kimataifa kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii nchini.
Alisema dhamira ya wizara ni kuongeza watalii kutoka milioni 1.5 hadi kufikia milioni tano kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyoelekeza ifikapo mwaka 2025.
Dk. Ndumbaro alieleza lengo la mkutano huo utakaofanyika kwa siku mbili ni kujadili namna ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa kuwakutanisha wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi.
Aliwataja baadhi ya washiriki wa mkutano huo ni wamiliki wa kampuni za kimataifa ya kutangaza utalii duniani na wataalamu kutoka Shirika la Umoja wa Kimataifa linaloshughulikia masuala ya utalii Duniani ( UN-WTO).
Akizungumzia washiriki hao, Dk.Ndumbaro, alisema mkutano huo wa kimataifa utatoa fursa kwa washiriki duniani kote na hata wale watakaoshindwa kufika nchini kushiriki kwa njia ya mtandao.
Akizungumzia sababu ya wizara hiyo kufanya mkutano huo, Dk.Ndumbaro alisema wameamua kufanya hivyo ili kuvitangaza vivutio vingi vya utalii na vya kipekee ambavyo havipatikani mahali popote duniani, lakini vimekuwa havijulikani kimataifa.
Dk. Ndumbaro alisema nchi ya Tanzania katika suala la vivutio vya utalii ipo vizuri ila katika suala la masoko ya vivutio vya utalii haipo vizuri.
Waziri huyo aliongeza kuwa uamuzi wa kufanya mkutano huo wa masoko na utalii ni moja ya mikakati maalumu ambayo kama Wizara ni kuhakikisha jitihada alizozianzisha Rais Samia za kutangaza utaliii nchini kupitia kipindi chake maarufu cha Royal Tour hazipoi na kusisitiza kuwa kampeni hiyo inazidi kuwa ya moto kila kukicha.
Dk. Ndumbaro alitoa wito kwa sekta binafsi kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha mkutano huo unafanyika ili sekta ya utalii iinuke tena, baada ya kushuka kutokana na ugonjwa wa Uviko-19.
Alieleza mkutano huo utakuja na mbinu mbadala kwa kuhakikisha sekta ya utalii nchini inapaa kwa kuyafanyia kazi mawazo yatakayotolewa haraka kadri iwezekanavyo ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Dk. Ndumbaro alisema kufanyika kwa mkutano huo kutasaidia kujua udhaifu katika kutangaza vivutio vya utalii.
NA MWANDISHI WETU



























