WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali itaendelea kupeleka fedha nyingi shuleni, ambapo amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kusimamia fedha hizo kwa umakini.
Majaliwa alisema ni wajibu wa watendaji wilayani na halmashauri kusimamia fedha kikamilifu zitekeleze majukumu yaliyokusudiwa kwa manufaa ya umma.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo, wilayani Nachingwea mkoani Lindi, wakati akizungumza na wanakijiji wa kata ya Chiumbati, baada ya kuweka jiwe la msingi la shule ya sekondari maalumu ya wavulana iliyojengwa wilayani humo kwa gharama ya sh. bilioni nne.
“Wanafunzi kubanana kwenye dawati moja hiyo ndani ya serikali ya awamu ya sita haitakuwepo kabisa na niwaombe wakuu wa wilaya, simamieni fedha za serikali zinazokuja ili kujenga shule zenu.
“Jitihada za serikali mnazoziona, wakurugenzi niwaombe kuweni makini sana katika matumizi ya fedha hizi, ili wanafunzi wetu wasome katika mazingira mazuri, yenye kuvutia ili wapate elimu bora,” alisema Majaliwa.

Aidha, alisema serikali inatekeleza sera nzuri ya elimu bila malipo, ambapo kutokana na utekelezaji wake, kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi shuleni na kusababisha uhaba wa rasilimali.
“Serikali ya awamu ya sita inataka kila mwanafunzi apate elimu iliyo bora na nimesikia hapa wavulana ndio walikuwa watoro sana kuliko wasichana, hivyo njia mliyoitumia ni nzuri na niwapongeze kwa kazi nzuri mliyoifanya ya kuanzisha shule ya wavulana,” alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Chionda Kawawa, akizungumza mbele ya Waziri Mkuu aliishukuru serikali kuendelea kutoa fedha nyingi katika sekta mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Lindi, ukamilishe upelelezi na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika katika tukio la wizi wa nondo 135 za mradi wa ujenzi wa wodi ya daraja la kwanza katika hospitali ya wilaya ya Nachingwea.
“Watu wote waliohusika na wizi wa nondo za ujenzi wa mradi huu wachukuliwe hatua haraka kwani tusipoanza kuwabana watu leo, wakatambua wajibu wao wa kuwatumikia wananchi miradi mingi ya maendeleo haitakamilika,” alisema.
Alitoa agizo hilo jana, baada ya kukagua mradi huo wa ujenzi wa wodi ya daraja la kwanza katika hospitali ya wilaya ya Nachingwea akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Lindi.
Pia, Waziri Mkuu alimuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Dk. Charles Mtabo, kuwa makini katika usimamizi na uendeshaji wa shughuli za afya, ili kuhakikisha malengo ya serikali kuhusu sekta hiyo yanafikiwa.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea Dk. Ramadhani Maiga alisema, mradi huo unaojengwa kwa awamu mbili unatekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri na mfuko wa jimbo kwa gharama ya sh. milioni 184.
Akizungumza na madiwani, watumishi wa umma na wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Nachingwea, aliwasisitiza kila mmoja atambue yupo wilayani humo kuwatumikia wananchi, hivyo atimize majukumu yake ipasavyo.
Waziri Mkuu alisema jukumu lake ni kuona kila agizo la Rais Samia linatekelezwa, ambapo amewataka watumishi hao wa umma wahakikishe uwajibikaji wao unakuwa na matokeo chanya.
Kadhalika, Majaliwa alitoa rai kwa madiwani wasimamie vyanzo vyote vya mapato na wahakikishe fedha zote zinazokusanywa zinaingia katika mfuko wa halmashauri.
Na SOPHIA NYALUSI, Nachingwea



























