KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo, amewajia juu watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma akiwataka kufanya kazi kwa maadili na weledi.
Mary alitoa kauli hiyo, alipofanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kutokana na uwepo wa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba, kuna watumishi wanaodai fedha wakati wa kutoa huduma.
Alisema hawatasita kuwachukulia hatua kwa mtumishi yeyote wa sekta ya ardhi, atakayebainika kuwadai fedha wateja kinyume na gharama halisi zilizowekwa na serikali kwa kisingizio cha fedha ya usafiri.
Mary alisema ofisi yake ilipokea taarifa kutoka kwa mwananchi mmoja akidai kutakiwa kutoa fedha kwa ajili ya usafiri wa kufuatilia hati, jambo alilolieleza kuwa halikubaliki kwa kuwa ni kuwatesa wananchi.
‘’Tunafuatilia kwa karibu wale wote wanaodai fedha kutoka kwa wateja maana hamjawekwa hapa kuwakandamiza wananchi na suala hili halikubaliki,’’ alisema.
Mary alisema, Wizara ya ardhi katika kuboresha huduma zake iko mbioni kukamilisha Kituo cha Huduma kwa Wateja, ambacho kitatumika kupokea changamoto na kero kutoka kwa wateja.
Akiwa Wilaya ya Kongwa, Mary alisalimia kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Kongwa, ambapo aliwaomba wajumbe wa baraza hilo kushirikiana na ofisi ya ardhi kuhakikisha vijiji ndani ya wilaya hiyo vinapangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuongezwa kasi ya utoaji hati za kimila.
Wilaya ya Kongwa ina vijiji 87 na kati ya hivyo ni vijiji 41 ndivyo vyenye mpango wa matumizi bora ya ardhi na kufanya vijiji 46 kusalia kupangiwa mpango huo.
Mary alisema wapo katika hatua za kukamilisha miradi mikubwa miwili ya Benki ya Dunia na mkopo wa Benki ya Exim, kwa lengo la kuhakikisha ardhi inapangwa na kupimwa na kufikia malengo ya kutoa hati 2,500, 000 katika kipindi cha miaka miwili.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Job Ndugai, alimshukuru Mary kwa uamuzi wake wa kuitembelea wilaya hiyo kwa lengo la kutatua changamoto zilizojitokeza.
Ndugai aliweka wazi kuwa moja ya changamoto kubwa katika wilaya hiyo ya Kongwa ni mashitaka yanayohusiana na migogoro ya ardhi.
Spika aliiomba wizara hiyo kuangalia namna ya kuipatia wilaya hiyo Baraza la Ardhi la Wilaya ili kuwaondolea usumbufu wananchi kufuata huduma za Baraza Dodoma mjini.
Na Mwandishi Wetu, KONGWA



























