UMOJA wa Wanawake Wenye Ulemavu wa Viungo Temeke (UWAVIUTE) nchini, umewataka wanawake wenye ulemavu kutosikiliza maneno ya upotoshaji dhidi ya chanjo ya Uviko-19, badala yake wajitokeze katika vituo vilivyotengwa ili wakachanjwe.
Kauli hiyo imetolelwa na mwenyekiti wa umoja huo, Albetina Mbachi, alipozungumza na UhuruOnline Jijini, Dar es Salaam.
Amesema watu wenye ulemavu ni kundi muhimu ambalo halitakiwi kukaa pembeni katika mapambano dhidi ya vita vya Uviko-19.
Albetina amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kutoa fedha kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zilizoelekezwa katika kila mikoa nchini.
“Sasa hivi suala la chanjo ni muhimu sana,watu wenye ulemavu tusibaki nyuma Rais wetu ametuletea chanjo tujitokeze kwa wingi tuache maneno ya upotoshaji,”alisema.
Albetina ameiomba serikali kuangalia kwa jicho la tatu utolewaji wa mikopo ya asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu, bado unasuasua hawapati kwa wakati.
Albetina amesema mikopo hiyo itolewe fedha badala ya vifaa ili kila mmoja abuni biashara nyingine itakayompa kipato kwa urahisi.
Albetina ametoa rai kwa watu wenye ulemavu kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na kuacha kuwa tegemezi ili kumuunga mkono Rais Samia.
“Rais Samia anafanya kazi vizuri, serikali yake ipo vizuri watu wenye ulemavu tumuunge mkono kwa kuchapa kazi kwa bidii,tujitume ili kuleta maendeleo na tuzidi kuondokana na ile hali ya mtu mwenye ulemavu ni tegemezi kwa familia,” alisema.
Na IRENE MWASOMOLA



























