MKUU wa Majeshi ya Ulinzi Generali Venance Mabeyo, ameviagiza vikosi vyote vya Jeshi la kujenga Taifa Nchini kuendelea kubuni miradi itakayoongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali pamoja na miradi ya biashara ili kuliwezesha taifa kuwa na usalama na uhakika wa chakula.
Generali Mabeyo ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati akizindua kituo kipya cha kisasa cha burudani cha Jeshi la Kujenga Taifa Makao Makuu ya nchi na ukumbi mpya wa mikutano na shughuli za kijamii, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi waandamizi wa Jeshi.
Amewaagiza kubuni miradi kama ambavyo wameendelea kubuni miradi mizuri hasa katika kilimo na ufugaji jambo ambalo litasaidia kwa majeshi kujitegemea.
“Ninaomba miradi hiyo iwe endelevu na ili kufikia lengo la kuhakikisha kuna kuwa na usalama na uhakika wa chakula.
“Niendelee kuwataka muwe wabunifu zaidi kwani fulsa zipo nyingi ambazo zinaweza kuwanufaisha katika kilimo na ufugaji kwani bado kuna ardhi ya kutosha ambayo itawezesha kupatikana kwa mapato ya kujitegemea na kuhakikisha wanakuwa na miradi mingi inayozalisha na waagiza kukamilisha kwa wakati baadhi ya majengo ambayo bado,”aamesema
Amesema kuwa mpaka sasa wana mashamba na skimu za umwagiliaji Chita Morogoro na mashamba ya mazao Mahindi na Maharage mikoa ya nyanda za juu kusini na mkoa wa Katavi na wameanza kujihusisha na kilimo cha mda mrefu na mfupi.
Awali Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajab Mabele, alisema kupatikana kwa eneo hilo ni utekelezaji wa maagizo ya mkuu wa majeshi katika kubuni vyanzo tofauti vya mapato ili kuepuka utegemezi kutoka serikali kuu.
Naye Brigedia Generali Mabena amebainisha kuwa mpaka sasa miondombinu ya eneo hilo imetumia Sh. bilioni 1.9 ikiwa ni ujenzi wa jengo la utawala, ukumbi, uzio na taratibu za ujenzi pia kwa majengo ambayo hayajajengwa yatagharimu zaidi ya sh.bilioni 1.2 na kwa ujumla miondombinu hiyo itagharimu zaidi ya bilioni 3.1 na kwamba JKT wapo tayari kupokea mapendekezo yatakayotolewa na wadau ili kuboresha zaidi huduma katika eneo hilo.
Ukumbi huo wa burudani uliozinduliwa una uwezo wa kubeba watu 1000 hadi 1200 kwa pamoja na kuwa na burudani mbalimbali amesema jengo hilo ni ubunifu mkubwa hivyo inatakiwa litunzwe ili liwe endelevu sambamba na kutoa huduma bora.
Na Happiness Mtweve,Dodoma



























