WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, amewasisitiza wananchi kuendelea kupata chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19.
Mazrui aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja wa waandishi wa habari kuhusu uhamasishaji wa chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19, uliofanyika Kariakoo, Unguja.
Alieleza kuwa chanjo ya Uviko-19 ni mkakati muhimu wa kupambana na ugonjwa huo ikizingatiwa kuwa bado upo na unaleta athari kwa jamii.
Alisema katika wimbi la tatu la ugonjwa huo, kati ya watu 70,000 waliopimwa takriban 1,400 walikutwa na maambukizi, hali inayoonyesha uwepo wa tatizo hilo.
Waziri huyo alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja ya kuhakikisha kuna nguvu ya pamoja kati ya wananchi na serikali kwa kushiriki kupata chanjo.
“Utoaji wa huduma za chanjo ni mkakati muhimu wa kuikinga jamii dhidi ya ugonjwa huo na Wizara yangu kupitia mpango wa chanjo imejizatiti ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa walengwa,” alisema.
Alisema serikali imeongeza vituo vya kutoa chanjo hiyo kutoka kimoja kilichokuwepo Lumbumba hadi kufikia 38.
Mazrui alisema tafiti mbalimbali zimefanyika na utoaji wa chanjo dhidi ya Uviko-19 pamoja na kuzuia vifo vinavyotoka na ugonjwa huo.
“Serikali baada ya kujiridhisha kwa kina na kupokea ushauri kutoka kamati mbalimbali nchini, imeamua kuanzisha chanjo dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19 ili kuongeza juhudi za kudhibiti ugonjwa huu,” alisema.
Alisisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama, ina ufanisi na ubora wa kumkinga binadamu dhidi ya Uviko-19 na ni muhimu kwasababu zinazuia watu kupata ugonjwa mkali, kulazwa na vifo.
Hata hivyo, alisema pamoja na kuongeza vituo kwa kila wilaya, bado mwamko kwa wananchi upo chini huku kukiwa na idadi ndogo sana kwa baadhi ya wilaya kwa wanaojitokeza kupata huduma.
Naye Kaimu mkurugenzi wa mradi wa chanjo MCGI, Dk. Mary Rose Giattas, alisema virusi vinavyosababisha Uviko 19 vina uwezo wa kujibadilisha na kusababisha madhara zaidi, hivyo wananchi wana wajibu wa kuthamini uwepo wa chanjo na kujitokeza kupata huduma.
Alisema chanjo hiyo ni salama, imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani(WHO) kupitia wataalamu wake, hivyo aliwaomba wananchi kutumia fursa hiyo kupata chanjo kwa hiyari.
Na EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBAR



























