IKIWA zimebaki siku tatu ili kushuka dimbani katika mchezo kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2022, dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Kim Poulsen amesema kikosi chake kipo kamili kwa ajili ya mchezo huo.
Taifa Stars itawakaribisha DRC mechi ya marudiano itakayopigwa Alhamisi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini.
Baada ya mchezo huo, Taifa Stars itasafiri kwenda Madagascar kucheza mchezo wa marudiano utakaopigwa Novemba 14, baada ya kushinda nyumbani 3-2, Septemba mwaka huu.
Akizungumza baada mazoezi yanayoendelea katika Uwanja wa Mkapa, Kim alisema wachezaji wake wote wapo vizuri na wana morari yakutosha kuelekea katika mchezo huo.
Alisema anajua Congo watakuja wakiwa wamejipanga ili kuhakikisha wanapata matokeo, lakini ana imani timu yake itafanya vizuri ili kuibuka na ushindi nyumbani.
Alisema amekuwa akiwafundisha wachezaji wake mbinu mbalimbali ikiwemo kupiga pasi ndefu, ili yeyote atakayekuwa na umiliki wa mpira aweze kufunga, anafanya hivyo ili kuwajengea uwezo wachezaji wake kufunga mabao ya mapema.
“Timu yangu imejipanga vizuri kwani wachezaji wana kiu ya kupata ushindi, nimewajenga kuanzia katika safu ya ulinzi hadi ushambuliaji, pia tutacheza kwa kushambulia na kupiga pasi za mbali ili kuhakikisha tunapata mabao ya mapema na kujiweka katika nafasi nzuri,” alisema Kim.
Kim alisema, anataka kushinda michezo yake yote miwili ambapo ataanza na DRC, baada ya hapo atamalizana na Madagascar ugenini.
Alisema anaamini watapata matokeo mazuri katika mechi mbili zilizobakia katika hatua ya makundi na kuingia hatua ya mwisho ya mtoano ambayo itazikutanisha timu 10 ili kupata timu tano zitakazoiwalikilisha Afrika katika michuano ya Kombe la Dunia mwakani.
Nahodha Msaidizi, John Bocco alisema wanaendelea kufanya maandalizi ya mwisho kuelekea katika mechi mbili zilizobaki, wachezaji wote wana morali ya kupambana ili kupata matokeo mazuri yatakayowasaidia kusonga mbele.
Alisema ushindi watakaoupata katika mechi mbili zilizobaki, sio wao peke yao bali ni ushindi wa mashabiki wa soka na Watanzania kwa ujumla.
Alisema wanatarajia kuzingatia kila mbinu ambazo walipewa na Kocha Kim, ili kuhakikisha wanapata ushindi na kuendelea kupaisha soka la Tanzania.
“Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda mchezo dhidi ya DRC na Madagascar, tunatambua umuhimu wa mechi hizo na kwamba tunaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili kutupatia sapoti ya kufanya vyema.
“Ushindi tutakaoupata sio wa timu pekee, bali ni kwa ajili ya mashabiki wa soka na Watanzania kwa ujumla, hivyo kila mchezaji anatambua anachotakiwa kufanya ndani ya uwanja,” alisema Bocco.
Alisema mashabiki ndio muhimili mkubwa kwao kwani wao watawapa nguvu na ujasiri wa kuhakikisha wanawamaliza Wacongo mapema.
Katika msimamo wa kundi J, Taifa Stars ipo kileleni kwa pointi saba sawa na Benin ambazo zinapishana mabao ya kufunga, ikifutia DRC yenye pointi tano wakati Madagascar ikiburuza mkia kwa pointi zake tatu, timu zote zikiwa zimeshacheza mechi nne kila moja.
Na NASRA KITANA