VIATU ni moja ya kitu muhimu kwa binadamu yeyote, kwani licha ya kutumika kama kifaa cha kuhifadhia miguu hata katika ulimwengu wa mitindo hutumiwa kama pambo la kunogesha mwonekano wa mtu.
Viatu huvaliwa na mtu yoyote bila kujali umri au jinsia kwa sababu hata wataalamu wa afya wamekuwa wakishauri kutunza miguu kwa kuiweka katika mazingira ya usafi.
Utunzaji wa miguu kwa kutumia viatu, husaidia kuiepusha miguu kupata maradhi ya ngozi yatokanayo na fangasi, bakteria baada ya kukanyaga uchafu.
Aidha ni wazi kuwa huwezi kuvaa nguo yoyote bila ya kupangilia na kujitathimini ni aina gani ya viatu utavaa kwa kuzingatia nguo uliyoandaa kulingana na mahali husika unapokwenda.
‘Slipppers’ ni moja ya viatu pendwa vinavyotumiwa na wanaume na wanawake, wakati wote humfanya mtu apendeze na kuwa huru kutokana na wepesi na uhuru anaoupata mtu pindi anapovaa.
Awali viatu hivi, vilionekana kutumiwa zaidi na watu wakati wa mapumziko nyumbani lakini kadri siku zinavyozidi kwenda, wabunifu wamekuwa wakiongeza thamani kwa kubuni zaidi jambo ambalo limewafanya watu kutumia viatu hivyo hata wanapokwenda katika shughuli za kawaida za kijamii na safari binafsi.
HISTORIA YAKE
Viatu hivyo vilianza kuvaliwa huko barani Asia katika karne ya 12, baada ya kubuniwa na Alvin Slipper, katika kipindi cha mwaka 1478 na baadaye vilianza kuvaliwa huko nchini China.
Pia viatu hivyo, vilipata umaarufu zaidi katika ulimwengu wa mitindo katika karne ya 18 mara baada ya wanawake kuvitumia mara kwa mara wakati wa shughuli za nyumbani.
Aidha, nchini Ufaransa viatu hivyo vilitumika zaidi na wakulima wakati wakiwa shambani.
WAPI UVAE
‘Slippers’ unaweza kuvaa wakati wa mapumziko nyumbani, katika fukwe za bahari, matembezi ya kawaida ikiwemo sokoni na safari za aina mbalimbali.
Pia ‘Slippers’ unaweza kuvaa kanisani, katika sherehe tofauti tofauti ikiwemo ya harusi, kitchen party na siku ya sherehe za kuzaliwa.
NINI UVALIE
Viatu hivyo unaweza kuvalia na nguo ya aina yeyote ikiwemo gauni, kaptula, sketi na blauzi, suruali ya jeans na nyinginezo.
Na IRENE MWASOMOLA