MENEJA wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya Ziwa Mashariki, Sophia Mziray, amesema kwa mujibu wa tafiti kutoka shirika la afya duniani (WHO), magoniwa yanayosababishwa na matumizi ya bidhaa zitokanazo na Tumbaku ni kisababishi namba mbili cha vifo vyote ambavyo vinatokea duniani huku watu wanaotumia bidhaa hizo wakiwa kwenye nchi zinazoendelea.
Ameyasema hayo katika kikao kazi cha watendaji wa sekta ya afya ngazi ya Halmashauri na mkoa wa Simiyu juu ya udhibiti wa bidhaa za tumbaku kilichofanyika mjini Bariadi na kueleza kuwa kutokana na matumizi ya bidhaa hizo za tumbaku kuna hatari kubwa zaidi ya kupata athari zitokanazo na bidhaa hizo huku akiongeza kuwa kwa mujibu WHO matumizi ya bidhaa hizo yameongezeka kwa kasi kubwa.
“Tulikuwa tunalitizama kwa mtazamo wa uzalishaji zaidi, kulizalisha na kutoa hamasa kwa watu ili waweze kuzalisha bidhaa za tumbaku, lakini shirika la afya duniani katika kufanya tafiti zake likabainisha hizi bidhaa za tumbaku matumizi yake yameongezeka kwa kasi kubwa sana” amesema Mziray
“Kama tunasema bidhaa hizi zinatumika sasa hivi kwa wingi sana katika nchi zinazoendelea, kwa hiyo maana yake sisi tupo katika athari kubwa ya kuweza kupata magonjwa haya ambayo kama tunavyofahamu ni magonjwa ambayo yana gharama kubwa katika matibabu yake kama magonjwa ya kansa.
kwa maana kama ni nchi pia yanaweza yakaleta athari kubwa na kudhorotesha uchumi wa nchi, na tumeshaandaa mpango kazi wa miaka mitatu ambao utatuwezesha kufikia lengo ambalo ni kulinda afya ya jamii”. ameongeza Mziray.
Awali akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, Katibu Tawala wa mkoa huo, Prisca Kayombo, amesema mkoa huo upo tayari kutekeleza maelekezo yote kwa ajili ya udhibiti wa bidhaa za tumbaku huku akiwaelekeza viongozi, wafanyabiashara na wenye mamlaka mbalimbali kuzingatia sheria na kutekeleza kama inavyopaswa.
“Maeneo yote ambayo bidhaa za tumbaku haziruhusiwi kutumika wekeni mabango kama nilivyoelekeza huu ni msisitizo.. makatazo kwa yale maeneo yasiyoruhusiwa basi wamiliki wahakikishe uvutaji wa sigara hizi unafanyika kwenye maeneo yaliyotengwa tu, nawasihi ndugu zangu na kuwataka wote wanaomiliki majengo yanayotumiwa na watu wengi, kuweka mabango kama sheria inavoelekeza, uwekaji wa haya mabango sio kwamba ni amri tu ni sheria imeelekeza kuweka hivyo.” amesema Kayombo.
Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa wa Simiyu Boniface Marwa amesema madhara ya matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku ni mengi ikiwemo saratani huku diwani kutoka kata ya Somanda Robert Rweyo akitoa ushauri kwa TMDA ,wizara ya afya kwa kushirikiana na wizara ya elimu kuanzisha mtaala kwenye shule ili wanafunzi wajifunze madhara ya bidhaa hizo tangu wakiwa wadogo.
Na Anita Balingilaki ,Simiyu



























