BALOZI wa Marekani Nchini Tanzania, Donald Wright, ameahidi kusaidia programu mbalimbali za habari ili kulinda uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari Tanzania.
Amesema hayo wakati alipotembelea klabu ya waandishi wa habari ya Mkoa wa Mwanza (MPC) na kufanya mazungumzo mafupi na viongozi wa Klabu.
Awali akitoa neno la utangulizi Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko alieleza changamoto za waandishi wa habari Tanzania ikiwemo uhitaji wa mafunzo, usalama na mazingira rafiki ya kufanyia kazi.
Akijibu baadhi ya changamoto hizo Balozi Wright alieleza kuwa atahakikisha anasaidia kundi la waandishi wa habari ili kuendeleza mazingira rafiki kwa vyombo vya habari.
Wright alisisitiza kuwa atakaa na wataalamu wake waliopo Jijini Dar es Salaam ili kuona uwezekano wa kusaidia baadhi ya programu za kuwajengea uwezo waandishi wa habari.
“Yote yaliyosemwa na MPC juu ya changamoto zinazowakabili waandishi wa Habari, nitahakikisha nazifanyika kazi hivyo nawaahidi kuwasaidia” Alisema Balozi Wright.
Mwenyekiti wa MPC Bwana Edwin Soko amesema kuna uhitaji mkubwa wa waandishi wa habari kijengewa uwezo kwenye maeneo muhimu kama usalama wa kimtandao kwa waandishi wa habari.
Pia aliweka wazi juu ya changamoto ya takwa la kisheria ya ukomo wa elimu uandishi wa habari na kutoa pendekezo la kutazamwa upya kwa sheria hiyo huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2017.
Na Blandina Aristides, Mwanza





























