NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amesema kwa sasa Shirika la Reli Tanzania (TRC) linakabiliwa na uhaba wa mabehewa ya abiria na mizigo.
Waitara ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi.
Katika swali lake, Mbunge huyo alihoji, ni lini tatizo la upungufu wa mabehewa ya abiria na mizigo litatatuliwa katika Kituo cha Mpanda?.
Akijibu swali hilo, Waitara alisema ili kuondokana na changamoto ya upungufu wa mabehewa katika kituo cha Mpanda na sehemu zingine, Shirika linaendelea na ukarabati wa mabehewa na tayari limesaini mkataba wa ununuzi wa vipuri kwa ajili ya ukarabati wa mabehewa 37 ya abiria na 600 ya mizigo.
Aidha, alisema mwezi Juni, 2021 Shirika limesaini Mkataba wa ununuzi wa mabehewa mapya 22 ya abiria utakaotekelezwa kwa kipindi cha miezi 12.
“katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 18.8 kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa mapya 100 ya mizigo,”alisema.
Alimwomba Mbunge huyo pamoja na wananchi wa Mpanda kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na zoezi la ukarabati na ununuzi wa mabehewa ya abiria na mizigo.
“Ni matumaini yetu kuwa pindi mabehewa yatakapowasili nchini na ukarabati kukamilika, tatizo la uhaba wa mabehewa kwa sehemu kubwa litakuwa limepatiwa ufumbuzi.” alisisitiza.
Na MWANDISHI WETU, DODOMA



























