BUNGE limeelezwa Katika mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya Tsh. bilioni 1.2 zimetengwa kwa ajili ya Ujenzi wa barabara ya Kolandoto hadi Meatu kwa kiwango cha lami.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameitoa kauli hiyo bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo(CCM).
Katika swali lake, Mbunge huyo alihoji ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kolandoto hadi Meatu?.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema Barabara ya Kolandoto – Mwanhuzi (Meatu) yenye urefu wa kilometa 117.57 ni sehemu ya mradi wa Barabara ya Kolandoto – Lalago – Mwanhuzi – Sibiti – Oldeani B Junction (km 328) usanifu wake ulikamilika mwaka 2017.
“Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami,”alisema.
Alibainisha kuwa wakati serikali ikiendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, Wizara hiyo kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.
Na Mwandishi wetu, Dodoma





























