SIKU moja baada ya wanafunzi wa kidato cha nne kuanza mitihani yao ya taifa, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde, amewatahadharisha kuepuka vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kusababisha wafutiwe matokeo yao.
Pia amewataka walimu kuwapa uhuru watahiniwa hao, ili wajipime kwa yale ambayo wamewafundisha katika kipindi cha miaka minne, na kwamba atakayekwenda kinyume na kanuni na sheria atachukuliwa hatua kali.
Akizungumza na UhuruOnline, Dk. Msonde amewataka wanafunzi kukataa ushawishi wa kupewa majibu ya mtihani kutoka kwa mtu yeyote, ili wasiharibu mitihani yao, bali watoe taarifa za yeyote anayetaka kuwaingiza katika mtego huo wa udanganyifu.
“Mwanafunzi yeyote ajiepushe na mitego ya udanganyifu hata kama ni mwalimu wake anaye mshawishi, asikubali kwa kuwa madhara yatakayo mkumba yataathiri matokeo yake,” alisisitiza
Aliwataka wanafunzi kutoa taarifa zozote za udanganyifu atakazo kutana nazo katika ofisi za kata, Halmashauri au kwa kuwasiliana naye kwa njia ya simu 0768 239 239 iliwaweze kuwachukulia hatua watakao bainika.
“Walimu waache wanafunzi wao wafanye mitihani yao kwa uhuru kwa kuwa mitihani hiyo inatokana na yale yote waliyowafundisha hivyo hawana haja yakuwa na wasiwasi.
“Kamati zetu za mikoa na halmashauri ziendelee kufanya kazi nzuri ya usimamizi kama walivyoanza leo, kwa kuwa kwa taarifa tulizonazo mpaka sasa watahiniwa wote wameanza mitihani yao vyema kwa kufikika katika maeneo yao kwa wakati,” alisema.
Aliwataka wazazi kuwapa ushirikiano watoto wao katika kipindi hiki kwa kuwapa muda wa kutosha wa kupumzika na kujiandaa vyema.
“Mtihani umeanza leo Novemba 15, unatarajiwa kumalizika Desemba 2, mwaka huu, hivyo wanafunzi waendelee na utulivu walioanza nao leo,” alisema.
UhuruOnline imepita katika shule mbalimbali za sekondari jijini Dar es Salaam, zikwiemo Benjamin Mkapa, Uhuru Mchanganyiko na Mnazi Mmoja na kushuhudia hali ya utulivu na usalama zikitawala.
Na SUPERIUS ERNEST



























