ZIKIWA zimetimia siku nane tangu atue nchini, kukinoa kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha mpya wa Simba, Pablo Franco, amesema ana matumaini hatakuwa na kazi ngumu ndani ya kikosi hicho kutokana na kuwa na wachezaji wengi wenye kiwango bora.
Pablo amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akirithi mikoba ya Mfaransa, Didier Gomes, ambaye aliamua kuachia ngazi baada ya timu hiyo kushindwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Akizungumza na UhuruOnline, Kocha Franco alisema baada ya kukinoa kikosi chake, ameshuhudia kuna wachezaji wazuri ambao ameanza kuwanoa na ana matumaini kwamba hatatumia nguvu kubwa kuwaweka katika muunganiko anaoutaka.
Alisema tangu ameanza kukinoa kikosi cha Simba, amegundua kwamba hatakuwa na kazi kubwa katika kutafuta kikosi cha ushindani kwani wachezaji wote wanaonekana wapo vizuri, hivyo kuna vitu vichache vya kurekebisha.
Pablo alisisitiza, kikubwa ambacho anahitaji kukifanya zaidi ndani ya kikosi chake, ni kuhakikisha anajenga muunganiko utakaofanya timu icheze kwa maelewano katika msimu huu kuanzia mechi inayofuata.
“Najua falsafa ya Simba ni kupiga pasi nyingi, hilo ni jambo kubwa ambalo ninatakiwa kulifanyia kazi mapema, hivyo baada ya kuwaangalia wachezaji wote nimegundua kwamba sitatumia nguvu nyingi kupata muunganiko ninaoutaka.
“Ninatarajia kikosi kitapata muunganiko mzuri mapema kwani wachezaji wanaonekana kuwa katika kiwango bora kwa sasa, hivyo kuna vitu kidogo cha kurekebisha ili kuhakikisha timu inakuwa tishio msimu huu,” alisema kocha huyo.
Hata hivyo kocha huyo raia wa Hispania aliongeza kuelekea mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting, wanaendelea na maandalizi huku akiwasoma wapinzani wao kujua mbinu zao.
Alisema ameshawaona wapinzani wake katika baadhi ya mechi walizocheza awali msimu huu na kwamba anajipanga kuwakabili na kuhakikisha anaibuka na ushindi.
Aliongeza, hana wasiwasi na mchezo huo kwani ndio utakuwa kipimo tosha kwa ajili ya kuangalia wachezaji wake na kuona wapi anatakiwa kuongeza nguvu zaidi katika mbinu zake ili timu iwe tishio zaidi.
Simba walianza ligi kwa suluhu dhidi ya Biashara United, wakashinda bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, wakaichapa bao 1-0 Polisi Tanzania, wakatoka suluhu dhidi ya Coastal Union kabla ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo.
Katika msimamo wa ligi Simba SC ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 11 baada ya kushuka dimbani mara tano, imeshinda michezo mitatu na kutoa sare mbili.
Na NASRA KITANA