BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora, limeazimia kufukuzwa kazi Mtumishi wa Idara ya Maabara wa Kituo cha Afya Mazinge, Godfrey Mwanyika, kwa tuhuma za kuiba kifaa cha hospitali (darubini).
Akitoa taarifa ya maazimio hayo yaliyofikiwa baada ya baraza kukaa kama Kamati ya Nidhamu, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Rashid Magope, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya mtumishi huyo kukiuka maadili ya utumishi wa umma.
Alisema mtumishi huyo alikamatwa na kifaa hicho maeneo ya nyumbani kwake wilayani humo, huku akijua kuwa kumiliki mali ya Halmashauri ni kinyume na utaratibu na ni kosa la jinai.
Kwa mujibu wa Magope tume iliundwa na kuchunguza suala hilo na mtuhumiwa akafikishwa mahakamani.
Hata hivyo, alisema Mahakama ilimwachia huru mtuhumiwa huyo, baada kukosekana ushahidi wa kutosha.
“Baada ya kurejea suala lake lilirudishwa katika Mamlaka ya Nidhamu kutokana na mwenendo wake unaotia mashaka, ikiwemo kuwahi kutuhumiwa kutoboa dari la ofisi ili kuingia chumba chenye dawa kwa nia ya kuiba,” alisema.
Aliongeza kuwa: “ Pamoja na mtuhumiwa kusamehewa katika tukio hilo la kujaribu kuiba dawa, uadilifu wake kama mtumishi wa umma unatia mashaka, ndiyo maana alisimamishwa kazi na sasa wameazimia afukuzwe moja kwa moja.”
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mayeka Tungu, alisema hakuna diwani anayependa mtumishi yeyote wa Halmashauri kufukuzwa kazi ila inapobainika tabia na mwenendo wa mtumishi fulani hauridhishi watachukua hatua.
Alisisitiza kuwa baraza halipo kwa kumwonea mtu au kufukuza mtumishi ila kila mtaalamu anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia maadili na utaratibu wa utumishi wa umma na si kufanya ujanja ujanja ili kujinufaisha.
Aliwataka watumishi wa umma wote waliopewa dhamana ya kusimamia utoaji huduma kwa jamii, kutekeleza shughuli zao kwa uadilifu mkubwa na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kudhalilisha taaluma zao.
Alipotafutwa Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa Halmashauri hiyo, Nico Kayange ili kulitolea ufafanuzi wa kina suala hilo, alisema atatoa taarifa rasmi ya suala hilo na hatua zilizochukuliwa.
Na Allan Kitwe, Tabora



























