MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, amekabidhi leseni za uchimbaji wa madini ya dhahabu kwa Halmashauri za Bariadi Mji na Vijijini ili waanzishe migodi ya madini, kutoa ajira na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Kafulila amekabidhi leseni hizo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange na kuzitaka Halmashauri hizo kuongeza vyanzo vya mapato.
“Dhana ya serikali ni kuzalisha, kila mtumishi aangalie kwa kiasi gani atachangia uzalishaji, kila mmoja akitimiza wajibu wake tutafika mbali… endeleeni kusimamia sekta ya madini ili tufanye vizuri, mnaweza kutengeneza miradi ya kimkakati kwa ajili ya kuwa na vyanzo vya mapato vya uhakika” amesema Kafulila.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Khalid Mbwana, amesema wataingia mkataba na wachimbaji ili uzalishaji ukipatikana waweze kugawana sawa.
Alisema kupitia migodi hiyo serikali (Halmashauri) watabaki wasimamizi pamoja na kuwa waangalizi wa usalama na kwamba watatoa fursa za ajira kwa vijana na akina mama.
Awali Mkuu wa wilaya hiyo alizitaka Halmashauri hizo kuanza uchimbaji mara moja kwa sababu wasipofanya hivyo watanyang’anywa leseni baada ya siku 90 kutokana na kutoziendeleza kwa mujibu wa sheria ya madini.
Na Costantine Mathias, Bariadi



























