NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Christina Mndeme, amewahakikishia wanawake nchini, CCM itaendelea kulinda haki za wanawake na kuwakinga dhidi ya vitendo vya ukatili.
Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza katika kikao cha Shina Namba 3, Kijiji cha Lumbe, Kata ya Ukumbisigara, Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora.
Katika kikao hicho, wajumbe wa shina hilo wakati wakijadili ajenda ya ulinzi na usalama, walieleza kuibuka kwa matukio ya wanaume kuwapiga wake zao hadi kuwadhalilisha.
“Kumpiga mwanamke ni ushamba sio ujasiri. Mwanamke ukipigwa nenda kashitaki dawati la jinsia ili haki itendeke. Serikali ya CCM itaendelea kuwalinda na kuwakinga wanawake dhidi ya vitendo vya uzalilishaji.
Aliongeza kuwa: “Ukandamizaji dhidi ya wanawake umekwisha na mwanaume aliyempiga mkewe hadi kumdhalilisha hatua kali zitachukuliwa.”
Mndeme aliwataka wajumbe wa shina hilo na wazee kukemea vitendo hivyo na kusisitiza maadili ndani ya jamii.
Kadhalika, aliwataka wanaume ambao nao wana malalamiko kuhusu kunyanyaswa na wake zao, wakashitaki katika madawati ya jinsia badala ya kulalamika pekee.
CCM HAITAVUMILIA UHALIFU
Wakati akiwa katika kikao hicho cha shina, baadhi ya watu waliibuka wakidai kuondolewa katika maeneo ya hifadhi ya misitu na mapori ya akiba kinyume cha sheria.
Kufuatia malalamiko hayo, Mndeme alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Paul Chacha, kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo ambapo mkuu huyo wa wilaya aliwataka watu hao kueleza ukweli mbele ya kiongozi na sio uongo.
Alisema Rais ameamua Kijiji cha Lumbe ambacho kilikuwa ndani ya eneo la hifadhi, wananchi waendelee na shughuli zao na tayari ametoa sh. milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu.
Aidha, alieleza kuwa eneo linalojengwa zahanati nalo lilikuwa ndani ya hifadhi, lakini sasa eneo hilo lipo nje ya hifadhi.
“Hawa wanaosema wameondolewa katika maeneo yao waseme ukweli, hata wazee wa kijiji hiki wanafahamu kwamba hao sio wenyeji wa Kijiji cha Lumbe ni wavamizi. Walivamia maeneo ya msitu wakakata miti na huko ndiko yakawa maficho ya vikundi vya kihalifu,” alieleza.
Chacha alibainisha kuwa baadhi ya wavamizi hao walioshirikiana na raia wa kigeni walikuwa wakijishughulisha na matukio ya uporaji minadani, mauaji na wizi wa mifugo.
“Wahalifu hao waliiba ngo’mbe zaidi ya 300, tukaamua kufunga mipaka kuhakikisha tunawakamata. Tuliwakamata wakiwa na raia wawili wa kigeni pamoja na silaha za kivita,” alieleza mkuu huyo wa wilaya huku akiungwa mkono na wananchi wakazi wa kijiji hicho.
Baada ya maelezo hayo, Mndeme alionyesha kukerwa na watu hao waliovamia mkutano wa shina na kutoa madai yasiyokuwa na ukweli.
“CCM hakiwezi kubariki vitendo vya kihalifu, hatutabariki watu kufanya matukio ya uhalifu. Tuliahidi kutunza taifa na ndio sababu tupo salama,” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu CCM Tanzania Bara.
Aidha, aliuagiza uongozi wa Wakala wa Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), kuweka alama za mipaka kutenganisha maeneo ya wananchi na hifadhi ili kuondoa migogoro baina ya hifadhi na wananchi.
Katika hatua nyingine, aliwataka mabalozi kukemea vitendo vya rushwa katika kuelekea uchaguzi mkuu wa chama unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Mndeme alitoa agizo hilo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Wazee, Kata ya Zugimlole, Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kiongozi atakayebainika kutoa rushwa kwa lengo la kupata nafasi ya kuwania uongozi, CCM itachukua hatua kali ikiwemo kuliondoa jina la muhusika katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.
Pia, aliwaomba wazee wa baraza hilo kukemea makundi, kuchafua na vitendo vya kuwadhoofisha viongozi waliochaguliwa vinavyofanywa na watu wenye lengo la kuwania uongozi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kaliua (CCM) Aloyce Kwezi, aliishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.
Alisema wamepokea zaidi ya sh. bilioni nne kwa ajili ya miradi ya elimu, afya na ukarabati wa miundombinu ya barabara.
Na MUSSA YUSUPH, Tabora



























